• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Kuna dalili za machafuko ngomeni mwa Jubilee – Ripoti

Kuna dalili za machafuko ngomeni mwa Jubilee – Ripoti

Na WANDERI KAMAU

TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imezitaja kaunti nane, nyingi zikiwa ngome za chama cha Jubilee (JP) kuwa “maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na ghasia za kisiasa.”

Kaunti hizo ni Kiambu, Kilifi, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Baringo, Nakuru, Nyeri na Kakamega.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi Jumanne, Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Bw Hassan Mohamed (pichani), alisema kuwa hali hiyo imesababishwa na ongezeko la mikutano ya kisiasa ambayo imekuwa ikifanyika karibu kila wikendi.

“Tunafahamu kuwa wanasiasa wengi tayari wameanza harakati za kujitayarisha kuwania nyadhifa mbalimbali kwenye uchaguzi wa 2022. Hata hivyo, hatutawaruhusu kuendeleza matamshi ya chuki za kisiasa na kikabila,” akasema Bw Mohamed.

Alisema kuwa kampeni hizo hazimaanishi kuwa kiongozi yuko huru kusema lolote alitakalo bila kuzingatia athari zake.

Kutokana na hilo, tume hiyo ilisema kuwa itawatuma maafisa wake wa nyanjani katika kaunti hizo, ili kufuatilia kwa kina matamshi yanayotolewa na viongizi katika mikutano ya kisiasa.

Ili kufanikisha ukusanyaji wa ushahidi, ilitangaza kuongeza mashine 110 za kurekodi na kamera nane maalum kwa maafisa wa usalama katika kaunti hizo.

Mkuu huyo alisema kuwa hatua hiyo vilevile inalenga kuimarisha juhudi za kukusanya ushahidi, kwani kesi nyingi ambazo imekuwa ikiwasilisha mahakamani zimekuwa zikosa kufaulu kwa ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

“Mahakama zimekuwa zikitushinikiza kutoa mashine ambazo tulitumia kurekodia matamshi ya washtakiwa mbalimbali ambao tumewafikisha mahakamani. Tunataka kuhakikisha kuwa kesi tunazowasilisha zina ushahidi maalum, ili kuona washukiwa wanahukumiwa kulingana na ushahidi tunaowasilisha,” akasema Bw Mohamed.

Kauli hiyo inajiri huku majibizano ya kisiasa kati ya mirengo ya ‘Tanga Tanga’ na ‘Kieleweke’ yakizidi kuchacha, hasa kuhusu urithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Baadhi ya viongozi pia wamelaumiwa kwa kutoa matamshi yanayozilenga jamii mbalimbali.

Mwezi uliopita, tume hiyo ilimwagiza mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi kufika mbele yake baada ya kutuhumiwa kutoa matamshi dhidi ya jamii fulani.

Hata hivyo, mbunge huyo aliomba msamaha, ijapokuwa alipewa onyo dhidi ya kutoa matamshi mengine ya kichochezi.

Jana, tume pia ilisema kuwa imeanza kitengo maalum cha kuwanasa wale wanaoendesha matamshi kwa njia za mitandao ya kijamii.

Kitengo hicho kitakuwa kikifuatilia jumbe zinazoandikwa na watumizi wa mitandao.

Na ingawa ilikubali kwamba imekuwa vigumu kuwakabili wale wanaotoa jumbe hizo, ilisema imeanza ushirikiano na asasi kama Baraza la Vyombo vya Habari (MCK) ili kuzinasa hata vituo vya redio vya lugha za kiasili zinazotumika kuendeleza chuki za kikabila na kisiasa.

“Tunafahamu athari za mitandao ya kijamii katika kusambaza jumbe za chuki za kisiasa na kikabila. Tutakuwa macho kuwanasa wale wanaoweka jumbe hizo,” akasema.

Vituo vya redio vya lugha za kiasili vililaumiwa sana kuwa mojawapo ya sababu kuu ya kuzuka kwa ghasia za 2007/2008. Vingi vililaumiwa kwa kuendesha vipindi vyenye chuki za kikabila, hali iliyochochea mapigano kati ya jamii mbalimbali.

You can share this post!

Wazito, Kisumu All Stars na Nairobi Stima zafukuzana...

KAMARI: Wafanyabiashara 17 wa kigeni wafurushwa

adminleo