Kuria apinga pendekezo la Duale kuondoa mfumo wa urais
Na NDUNGU GACHANE
MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria amepuuzilia mbali pendekezo la Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale, la kufanyika kwa kura ya maoni kwa lengo la kutupilia mbali serikali ya mfumo wa urais na badala yake kuchukua mfumo wa bunge.
Alisema kwamba pendekezo hilo haliwezi kufanikiwa ila tu iwapo maeneo bunge yote yanaweza kusawazishwa na kuwa na idadi sawa ya wapiga kura.
Bw Kuria alisema wapiga kura kutoka maeneo bunge yote ni sharti wawe na idadi sawa ya kura kwa sababu kulingana naye haitakuwa sawa kwa kiongozi aliyechaguliwa kuwa na eneobunge lenye wapiga kura 3,000 kumpigia kura Waziri Mkuu huku mbunge akichaguliwa na wapiga kura zaidi ya 100,000.
“Hatutawahi kamwe kuwa na mfumo wa Utawala wa Bunge Kenya isipokuwa kwanza tusawazishe maeneo bunge yawe na idadi sawa ya wapiga kura. Eneobunge la Bw Duale lina watu wanaoweza kutoshea katika mabasi mawili na anataka kujitoshanisha na wengine kutoka maeneo bunge yenye idadi kubwa ya watu. Haina maana na haitatendeka labda nikiwa nimeaga dunia,” alisema Bw Kuria.
Bw Duale alisema jamii ya wafugaji itaunga mkono wito wa kuwa na kura ya maoni ya kubuniwa kwa mfumo wa serikali ya bunge ili kuwapa watu kutoka kaunti zote nafasi sawa ya elimu, uchumi na biashara pamoja na kudhibiti visa vya ghasia baada ya uchaguzi.
“Tunapaswa kuanzisha mfumo wa serikali ya bunge ambao utakuwa na Waziri Mkuu atakayekuwa kiongozi wa serikali ili mtoto kutoka Garissa, Kisumu, Wajir, Turkana, Kiambu na Nairobi atapata nafasi sawa ya elimu, biashara na uchumi ikiwemo kukabiliana na ghasia za baada ya uchaguzi na kesi katika Mahakama ya Juu zinazoibua taharuki nchini,” alisema.
Bw Duale alipendekeza kwamba baada ya uchaguzi, chama kilicho na idadi kubwa zaidi ya wanachama katika Seneti au muungano ulio na idadi kubwa zaidi ya wanachama, utaungana na kumtoa Waziri Mkuu.
Anasema mfumo huo ndio bora kwa taifa hili na akatoa wito kwa Jopokazi la Building Bridges kupendekeza kufanyika kwa kura ya maoni ikiwa na pendekezo lake.