Habari Mseto

Kurukwa kipetero? Minong’ono washirika wa Gachagua, Gakuya na Mejja Donk wakikutana na Ruto

Na MOSES NYAMORI November 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WASHIRIKA wawili wa karibu wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumanne walihudhuria mkutano ulioitishwa na Rais William Ruto katika Ikulu, na kuzua mdahalo kuhusu msimamo wao wa kisiasa.

Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya na mwenzake wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru almaarufu MejjaDonk walihudhuria mkutano huo pamoja na Wabunge wengine wa Nairobi kujadili mpango wa kurejesha mto Nairobi miongoni mwa miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa kwa pamoja kati ya serikali ya kitaifa na kaunti chini ya Gavana Johnson Sakaja.

Viongozi hao wawili walipuuza mkutano sawa na huo ulioitishwa na Rais mnamo Septemba wakati wa kilele cha mzozo wake wa kisiasa na baadaye kuondolewa kwa Bw Gachagua.

Baadhi ya wanachama wa ODM pia walisusia mazungumzo hayo, ambayo yalijumuisha kuandamana na Rais kukagua Mradi wa Nyumba za bei nafuu wa Kibra, Soweto Mashariki.

Kando na wabunge hao wawili, viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho cha Ikulu ni pamoja na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, wabunge George Aladwa (Makadara), Mark Mwenje (Embakasi Magharibi), Peter Orero (Kibra), Anthony Oluoch (Mathare), Ronald Karauri (Kasarani), (Felix Odiwuor almaarufu Jalang’o (Lang’ata), Mwafrika Kamande (Roysambu), Tim Wanyonyi (Westlands), John Kiarie (Dagoretti Kusini) na Beatrice Elachi (Dagoretti Kaskazini).

Bw Gathiru aliambia ‘Taifa Leo’ kwamba ajenda ya mkutano huo haina uhusiano wowote na siasa. Pia alisema bado anasalia kuwa mwanachama wa UDA licha ya mzozo wa kisiasa kati ya Rais na Bw Gachagua.

Mbunge huyo pia alipuuzilia mbali madai kuwa kuwepo kwao katika mkutano huo ni ishara kwamba wanaweza kumtema Bw Gachagua, akisema kuwa “hakuna vile tunaweza kumuacha Gachagua, anabaki kuwa kiongozi wetu na watu wako pamoja naye, sio tu katika eneo la Mlima Kenya. lakini kote nchini.

“Sisi si maadui (na Rais). Tulitofautiana tu kwa maoni kuhusu kile kilichotokea. Unatakiwa kujua sisi ni wanachama wa UDA, tukiongozwa na Rais,” alisema.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA