Habari Mseto

LAMU: Washinikiza mafunzo ya mihadarati yajumuishwe kwa madrassa

January 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

BARAZA la wazee, miungano ya akina mama na vijana Kaunti ya Lamu yanashinikiza somo la dawa za kulevya, athari zake na jinsi ya kuepuka dawa hizo kujumuishwa katika silabasi ya mafundisho yanayotolewa kwenye madrassa mbalimbali na hata masomo ya watoto Jumapili makanisani kote Lamu.

Wazee, akina mama na vijana hao wanaamini somo hilo ambalo wanapendekeza liwe la lazima litasaidia kukabiliana na janga la mihadarasti ambalo linazidi kuathiri na kupoteza vijana wengi wa kaunti ya Lamu.

Wakizungumza wakati wa sherehe za kuukaribisha Mwaka Mpya katika ukumbi wa hoteli  ya Mwana Arafa mjini Lamu jana, wazee, akina mama na vijana waliokongamana walieleza hofu yao kuhusiana na jinsi idadi kubwa ya vijana ambao wangekuwa viongozi wa kesho  inavyozidi kuangamia kwa mihadarati.

Wakiongozwa na mmoja wa wazee, Feiswal Miji, wakazi hao walisema wakati umewadia kwa vituo vya madrassa na makanisa kote Lamu kujumuisha somo hilo la mihadarati ili kuwapa watoto ufahamu wa mapema kuhusu mihadarati, athari zake na jinsi watakavyokabiliana na msukumo wa marafiki katika maisha yao.

Bw Miji aliipongeza Wizara ya Elimu kwa kujumuisha mafundisho ya masuala ya mihadarati katika mtalaa wake wa elimu hapa nchini.

Alisema ili kupiga jeki mfumo huo, kuna haja ya shule za madrassa hasa kwa waislamu na pia shule za watoto za Jumapili makanisani kuhakikisha elimu ya mihadarati inapewa watoto ili wajue mapema na kuepuka hatari inayowakodolea macho maishani mwao.

Mwenyekiti wa Maendeleo ya Wanawake, Kaunti ya Lamu, Bi Fatma Salim akitoa hoja yake wakati wa kongamano la kufunga mwaka eneo la Mwana Arafa. Picha/ Kalume Kazungu

“Itakuwa bora kwa shule zetu za madrassa na hata makanisani kuhakikisha wanatoa elimu ya lazima kuhusu masuala ya mihadarati, athari zake na jinsi watoto wataepuka uozo huo wanapokua. Cha msingi  ni kuhakikisha mtalaa wa maddrassa na ule wa shule za Jumapili makanisani unajumuisha somo hilo mara moja hasa hapa Lamu. Tukifanya hivyo ninaamini tutaokoa kizazi chetu kisiangamia kwenye mihadarati,” akasema Bw Miji.

Mmoja wa wazee, Bw Mohamed Mbwana, alisema inasikitisha kuona kwamba kizazi ambacho kingesaidia kuleta maendeleo Lamu kinaangamia kwenye tatizo sugu la mihadarati.

Alipongeza pendekezo la kuanzishwa kwa somo hilo la lazima kwenye madrassa na makanisani ili kuokoa kizazi cha Lamu.

Naye Mwenyekiti wa Muungano wa Maendeleo ya Wanawake, Kaunti ya Lamu, Bi Fatma Salim, aliwataka wazazi kuwa mstari wa mbele katika kufuatia mienendo ya watoto wao ili wasiharibike kwa kujitosa katika janga la mihadarati.

Bi Salim pia aliitaka serikali kukaza kamba zaidi katika vita dhidi ya dawa za kulevya kote Lamu ili kuzuia kuingizwa kwa dawa hizo eneo hilo.

“Wakati umewadia kwa wazazi kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao ili kuepuka wasipotelee kwenye janga la mihadarati. Idara ya usalama pia itilie mkazo vita dhidi ya mihadarati ili dawa zozote zisiingizwe Lamu kuharibu vijana wetu,” akasema Bi Salim.

Katika ripoti ya hivi majuzi kutoka kwa idara ya usalama, Kaunti ya Lamu, miji ya Faza, Kizingitini, Mbwajumwali, Myabogi na Tchundwa ilitajwa kuwa baadni ya maeneo yanayaoongoza kwa vijana wengi wanaotumia mihadarati na kuhangaisha jamii eneo hilo.