Lipa ushuru namna unavyomwaga pesa, Mudavadi amwambia Ruto
Na PETER MBURU
UHASAMA wa kisiasa baina ya kiongozi ANC Musalia Mudavadi na naibu wa Rais William Ruto umezidi kutokota baada ya Bw Mudavadi kurusha kombora jingine dhidi ya hasimu wake, akikosoa matumizi ya pesa za misaada kwa wingi sana.
Katika mashambulizi hayo ya Jumatano, Bw Mudavadi bila kumtaja Bw Ruto moja kwa moja alidai kuwa kiongozi huyo anashindana na kampuni ya Safaricom kuchanga pesa za misaada, wakati zake hazijulikani zinapotoka.
Alihoji kuwa japo anajiita mfanyabiashara, hakuna kampuni yake hata moja ambayo inaorodheshwa kati ya zile zinazolipa ushuru mkubwa nchini, hivyo akishangaa kuhusu uhalali wa pesa hizo.
Kiongozi huyo aidha alisema kuwa suala zima la ukaguzi wa hali ya maisha ya maafisa wakuu wa umma lilifeli, kwani matunda yake hayajaonekana.
“Kama jamii tunafaa kuuliza na si tu kuhusu misaada kwa makanisa, tunafaa kuuliza kuhusu mambo ambayo ni wazi kabisa, ni Mkenya yupi huyu ambaye anachanga pesa kwa ushindani na Safaricom ambayo ndiyo kampuni tajiri sana nchini ilhali ukifuatilia wanaolipa ushuru mkubwa nchini, hakuna moja kati ya kampuni zake zilizoorodheshwa kuwa bora,” akasema Bw Mudavadi.
Katika mashambulizi zaidi, Bw Mudavadi kwenye mahojiano alimfananisha kiongozi huyo na ‘Anania’ wa Biblia ambaye alimhadaa Mungu kwa kuficha baadhi ya pesa alizouza mali yake, na akafa kutokana na hilo.
“Aliuza mali yake na akaenda kanisa kupeleka pesa hizo na mhubiri akamuuliza kwanini alipeleka pesa ambazo hazikuwa sawa na dhamana ya mali yenyewe, kwa kudanganya mungu, Anania alikufa,” akasema Bw Mudavadi, ambaye amekuwa akikosoa hali ya naibu wa Rais kuchanga pesa nyingi kila mara katika makanisa na hafla za Harambee.
Viongozi hao wawili hawajakuwa wakionana macho kwa macho, kwani wamekuwa wakivamiana kila wanapopata nafasi.
Wiki chache zilizopita, Bw Ruto alimkashifu Bw Mudavadi kuwa analewa kupindukia, akisema ni hali hiyo inayomnyima pesa za kuchangia watu ili wawe sawa.