Habari Mseto

LYDIA MUKAMI: Chipukizi mwenye ndoto ya kufikia upeo wa Oprah Winfrey

March 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

ANAORODHESHWA miongoni mwa waigizaji chipukizi humu nchini. Anaamini kwamba Wakenya wana uwezo wa kuzalisha filamu bora bila kutegemea wenzao kutoka nchi zinazoendelea.

Anadokeza kuwa waigizaji wa humu nchini wameiva vya kutosha kutengeneza filamu aina ya Afro Cinema za Kenya na kutwaa nafasi ya kazi za kigeni ambazo hurushwa kupitia Inooro TV na Kameme TV.

Kando na kuigiza demu huyu ni mwana mitindo na mtangazaji ambaye huandaa shoo iitwayo ‘Lets Talk’ ambayo huonyeshwa kupitia Ebru Televisheni hapa nchini.

Lydia Mukami maarufu kama KM anasema yeye ni mgeni katika masuala ya filamu lakini amepania kujituma kiume kuhakikisha amefikia kiwango cha waigizaji wa kimataifa miaka ijayo.

Akipiga soga na Taifa Leo Dijitali, alisema anatamani kuibuka mwigizaji bora kufikia kiwango cha staa na mtangazaji wa kimataifa Oprah Winfrey.

Aidha alisema angetaka zaidi kumiliki brandi ya kuzalisha filamu ili kusaidia waigizaji chipukizi nchini. Kadhalika analenga kuanzisha kipindi cha kujadili masuala ya kijamii katika kituo cha redio.

”Hakika ninaamini nimeiva kushiriki filamu za hadhi ya Hollywood,” alisema na kuongeza kwamba amepania kuanzisha miradi nyingi tu katika sekta ya burudani siku sijazo.

Dada huyu anawasuta Wakenya ambao wametekwa na filamu za kigeni na kuziponda kazi zilizotengezwa humu nchini. Picha/ John Kimwere

”Nilirejea hapa Kenya miaka michache iliyopita lakini nimegundua wapo wasanii wengi tu wa humu nchini wanaume na wanawake waliotuzwa talanta ya uigizaji ila hawajafanikiwa kuonyesha ubunifu wao kisanaa. Lakini binafsi ninahisi yapo masuala mengi yanayohitaji kutelekezwa kusudi kuinua tasnia ya filamu nchini.”

KM anasema Serikali inastahili kusapoti miradi ya wasanii ili kuunda nafasi za ajira kwa vijana kote nchini. Anaitaka Serikali ya kitaifa kufanya kazi sako kwa bako na serikali za Kaunti kwa kuwaleta pamoja waigizaji wote pia kupata maoni yao kuhusu taaluma hiyo.

”Kando na hilo Serikali inapaswa kuondoa ama kupunguza kodi ambayo hutozwa kampuni husika wakati zinaposhuti filamu katika miji tofauti nchini,” alisema na kuongeza kwamba mpango mwafaka kama huo umechangia tasnia ya filamu kupiga hatua kubwa nchini Nigeria.

KM anajivunia kushiriki muvi moja hivi karibuni iitwayo ‘Duty Call’ chini ya Onfone Media. Kwa upande wa uanamtindo anajivunia kuwepo katika picha za matangazo za VISA, Safaricom na NHIF mwaka 2018.

Anashauri waigizaji wanaoibukia kuwa wabunifu na kufikiria zaidi kuanzisha miradi mizuri pia kushirikiana kufanya kazi pamoja na wenzao ili kupata nafasi nzuri kulilia Serikali kuwapiga jeki.

Binti huyu anawataka waigizaji chipukizi kujitolea mhanga kushiriki majaribio mara nyingi tu bila kulegeza kamba na kuamini ipo siku watafanikiwa.

Pia anawahimiza kuwa wepesi wa kukubali kujifunza masuala tofauti kuhusu tasnia ya filamu ili kupata maarifa zaidi.