Maafisa watakiwa kuomba wakazi msamaha
Na KALUME KAZUNGU
BARAZA la wazee Kaunti ya Lamu linataka wakuu wa usalama Pwani waombe radhi kwa kuwadharau wakazi.
Mnamo Jumanne, Mshirikishi wa Usalama, Ukanda wa Pwani, Bw John Elungata, Kamanda Mkuu wa Polisi eneo la Pwani, Bw Mercus Ochola na maafisa wengine wakuu wa idara ya usalama eneo hilo walizuru Lamu ili kusikia maoni na vilio vya wakazi wa Lamu.
Walipofika Lamu majira ya adhuhuri, walifanya kikao na kamishna wa kaunti mjini Lamu hadi majira ya alasiri kabla ya kufika eneo la Mkunguni kuhutubia wakazi.
Ingawa wananchi walikuwa wamesubiri tangu asubuhi, walitarajia wangepewa nafasi kuwasilisha vilio vyao kwa maafisa hao wa umma ili kupata usaidizi.
Punde maafisa hao walipowasili Mkunguni, walihutubia wananchi kwa dakika 30 pekee na kuwataka waliokuwa na malalamishi wayawasilishe kwa ofisi ya Shirika la kutetea Haki za Waislamu (MUHURI), ambapo malalamishi yao yangewafikia mjini Mombasa.
Wazee wakiongozwa na Bw Mohamed Mbwana, walisema hawajaridhishwa na jinsi maafisa wa idara ya usalama walivyoshughulikia mambo yao.
Walisema badala ya maafisa wa usalama kushughulikia vilio vya wananchi wa Lamu, wao walidhihirisha jinsi wanavyowadharau wakazi wa eneo hilo kwa kudinda kuwapa sikio wakazi hao ili kuwasilisha malalamishi yao.
Wazee wanasema waliachwa pweke kinyume na matarajio makuu waliyokuwa nayo kuhusu ziara ya wakuu hao wa usalama eneo hilo.