Habari Mseto

Maandalizi ya mitihani ya KCPE na KCSE yako tayari – Amina

September 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

 Na OUMA WANZALA

MAANDALIZI ya mitihani ya kitaifa ya mwaka huu yamekamilika, Waziri wa Elimu Amina Mohamed ametangaza.

“Tumeweza kupata makontena mengine 40 na kuyapeleka katika baadhi ya maeneo ili yawe karibu na vituo. Wale walio na jukumu la kusimamia mitihani wanapaswa kuwa waangalifu ili kuhakikisha kuna matokeo mema,” alisema Bi Mohamed.

Imeibuka kuwa mkutano utakaoshirikisha Wizara za Elimu, Usalama wa Ndani na Wizara ya Tekinolojia utafanyika Septemba 17 ili kuweka mikakati ya kusimamia mitihani itakayoanza Oktoba.

Bi Mohamed alisema ni lazima mitihani ilindwe kwa vyovyote vile.

“Tunafaa kuhakikisha kuwa hakuna wizi wa mitihani. Walimu, wazazi na wadau wote katika sekta hii wanafaa kuwahakikishia watoto wetu ambao ni watahiniwa kwamba bidii huzaa matunda mema. Hivyo basi, ni jukumu la walimu kukamilisha mtaala kwa wakati ili wanafunzi wawe na ujasiri wanapojiandaa kwa mitihani,” alisema.

Alisema watahiniwa hujaribu kudanganya katika mitihani kwa kukosa kuandaliwa vyema.

“Wizara imejitolea kuhakikisha kiwango cha juu cha kusimamia mitihani,” alieleza Waziri Mohamed. Aliwataka wazazi na walimu kuanza kuwashauri wanafunzi wakiwa wadogo ili kuzuia visa vya ukosefu wa nidhamu shuleni.

“Mwaka huu, tulishuhudia visa vya ukosefu wa nidhamu katika shule zetu. Vitendo kama hivyo vya ghasia vinafaa kukomeshwa. Kama wizara, tutahakikisha watakaohusika watakabiliwa kisheria. Bodi za kusimamia shule, vyama vya wazazi na mabaraza ya wanafunzi zinafaa kuruhusiwa kutekeleza majukumu yao na wanafunzi kuonyeshwa mbinu za kuwasilisha malalamiko yao ili yatatuliwe,” alisema Waziri Mohammed.

Alisema hayo alipoongoza sherehe za 52 za kuadhimisha siku ya kusoma ulimwenguni zilizoandaliwa katika Kaunti ya Wajir Jumamosi.

Kulingana na Bi Mohammed, vituo vya elimu ya watu wazima vinapaswa kutumiwa kuwafunza wazazi maarifa ya ulezi na kuwaelekeza watoto wao kuwa na mienendo mizuri ili wakue wakiwa watu wakutegemewa.

“Ni kwa kuzingatia haya ambapo mtaala mpya unashirikisha mzazi katika elimu. Ninahimiza wazazi wote na walimu kutekeleza majukumu yao ya kukuza wanafunzi na wasiwaachie walimu majukumu yao,” alisema.

Siku ya kusoma ulimwenguni huleta pamoja wadau katika elimu kujadili mchango wao katika elimu na athari zake kwa ustawi wa kijamii na uchumi.

“Kenya imepiga hatua kubwa katika juhudi zake za kukabiliana na kutojua kusoma hasa kupitia mfumo wa elimu ya msingi na shule za upili za mchana kutwa bila malipo.

Mipango mingine ya kukabiliana na hali hii ni kupitia katiba inayosema kwamba kila mtu ana haki ya kupata elimu na kwamba kila mtoto ana haki ya kupata elimu ya msingi bila malipo,” alieleza Bi Mohamed. Alisema maeneo kame nchini yako nyuma katika kupigana na kutojua kusoma.