Madiwani kuamua iwapo referenda itafanyika
WANDERI KAMAU na CHARLES WASONGA
UAMUZI wa iwapo referenda ya ‘Punguza Mzigo’ itafanyika, sasa iko mikononi mwa madiwani katika kaunti zote 47.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati alisema tume yake imetosheka na saini 1,222,541 za wapigakura wanaotaka Katiba ifanyiwe marekebisho.
Baada ya saini hizo kudhibitishwa, hatua inayofuata kulingana na Katiba ni mabunge ya kaunti kuujadili na kuamua. Mchakato huo utachukua muda wa miezi mitatu na sharti upitishwe na mabunge 24 ya kaunti ili kupita hatua inayofuata.
Ukipita, maspika wa mabunge hayo watawasilisha maamuzi yao kwa maspika wa Seneti na Bunge la Kitaifa ili kujadiliwa.Ikiwa mabunge hayo mawili yataupitisha mswada huo, basi utawasilishwa kwa Rais kutiwa saini na kuwa sheria itakayotoa mwanya kwa maandalizi ya kura ya maamuzi.
Ni baada ya hapo, ambapo tume itaanza harakati za maandalizi ya kura hiyo.
Kati ya mambo ambayo ‘Punguza Mzigo’ inataka kubadilishwa ni Rais kuhudumu kwa muhula mmoja wa miaka saba na kupunguzwa kwa idadi ya maeneo bunge kutoka 210 hadi 94.
Pia Inapendekeza idadi ya masenata ibaki 47 lakini viti vya Wabunge Maalum na madiwani maalumu viondolewe, sawa na vya Wabunge Wawakilishi wa Wanawake.
Kulingana na Dkt Eukot, nyadhifa za Manaibu Gavana hazijakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na kwa hivyo zinafaa kuondolewa.
Pia, anaamini kuwa Bunge la Seneti lafaa kuwa na mamlaka makuu kuliko Bunge la Kitaifa na kwamba kitovu cha maendeleo chafaa kuwa Wadi.
Kwa sababu hiyo, ‘Punguza Mzigo’ inapendekeza Serikali za kaunti zitengewe asilimia 35 ya Mapato ya Kitaifa wala sio asilimia 15 ilivyo katika katiba ya sasa.
Pia inapendekeza kuwa mshahara wa Rais usizidi Sh500,000 kila mwezi na ule wa wabunge usizidi Sh300,000 kwa mwezi.
Mchakato wa ukaguzi wa saini ulianza mnamo Mei 28 mwaka huu na kumalizika mnamo Juni 26, katika Taasisi ya Mitaala Kenya (KICD).
Ukaguzi huo ulikuwa ukiendeshwa na kundi maalum lililowajumuisha wasimamizi 24 na makarani 125.
Mapendekezo hayo yana uwezo wa kuungwa mkono na Wakenya ambao wamechoshwa na gharama ya waliochaguliwa.