Magavana wataka Wizara ya Fedha ifuate maagizo
Na NDUNGU GACHANE
BARAZA la Magavana (COG) sasa linataka Wizara ya Fedha kuheshimu uamuzi wa Mahakama na kutuma mgao wa pesa kwa serikali za kaunti kwa wakati.
Baraza limeandikia barua waziri wa fedha, Ukuru Yattani likitaka afisi yake kuheshimu uamuzi wa korti wa kuiamuru itoe pesa kwa serikali za Kaunti.
Kupitia mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Wyciffe Oparanya, baraza linasema hatua ya serikali ya kuchelewesha kutoa pesa hizo kwa kaunti imelemaza huduma, kushindwa kulipa wafanyakazi na kutatiza upitishaji na utekelezaji wa miswada kadhaa.
‘’Baraza la magavana linasema serikali za kaunti zote 47 hazijapokea pesa za kila mwezi Desemba 2019 ambazo zilipaswa kuwa tayari kufikia Desemaa 15. Kutokana na hayo serikali za kaunti haziwezi kutimiza malengo yake yakiwemo kufanikisja miswada pamoja na kulipa mishahara ya wafanyakazi,” barua hiyo inasema.
Naibu wa mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Mwangi wa Iria alisema hatua ya wizara ya fedha kukosa kutekeleza agizo inatatiza wazazi wanaopeleka watoto wao shule muhula wa kwanza ukianza Jumatatu ijayo.
“Baraza la Magavana linaelezea wasiwasi kwamba Kaunti 47 ziko kwa shida kwani wanafunzi hawatapelekwa shuleni,” Bw Oparanya aliambia ‘Taifa Leo’.
Baraza linaweka matumaini katika agizo la korti lililotolewa na Mahakama Kuu mnamo Desemba 13 kulazimisha wizara ya fedha kutoa pesa hizo mara moja kwa kuzingatia kipengee cha 19 cha Katiba na kipengee cha 17 (6) cha Sheria ya Fedha za Umma.
Jaji Weldon Korir aliamuru wizara na mdhibiti wa bajeti kufuata sheria na kutoa fedha ifikapo tarehe 15 ya kila mwezi kwa mujibu wa Katiba.
Baraza la Magavana lilienda kortini mnamo Desemba 10, 2019, ili kupinga uamuzi wa wizara wa kuzuia fedha kwa Kaunti 17 ambazo hazikuwa zimelipa madeni.
Katika ombi hilo, COG ililaumu wizara kwa kukosa kutoa pesa hizo.
“Kulingana na kipengele cha 219 sehemu ya 17 (6) ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, washtakiwa wa kwanza na wa pili wana jukumu la kutoa pesa hizo wakati unaofaa kabla ya tarehe 15 ya kila mwezi,” unasema uamuzi ambao baraza inataja katika barua kwa wizara.