Habari MsetoKimataifa

Magufuli aagiza shule zifunguliwe mwezi huu

June 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli ameagiza shule zote kufunguliwa Juni 29, baada ya kufungwa kwa takriban miezi mitatu tangu Machi.

Uamuzi huu umefanya Tanzania iwe taifa la kwanza Afrika Mashariki kuagiza kufunguliwa kwa shule huku ikiendeleza shughuli nyingi nyingine kama kawaida licha ya janga la corona kutikisa ulimwengu mzima.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana alipokuwa akihutubia bunge jijini Dodoma.

Alisema hakuna haja ya kuendelea kufunga shule kwa sababu maambukizi ya virusi vya corona yamepungua sana Tanzania.

Mapema mwezi huu, vyuo vikuu, taasisi za elimu ya juu na wanafunzi wa Kidato cha Sita walirejea shuleni.

Ijapokuwa hivi majuzi Rais Magufuli alitangaza kuwa corona imeisha Tanzania akidai kuwa pana wagonjwa wanne pekee waliosalia, jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuna wagonjwa 66 hospitalini.

Kulingana naye, wagonjwa hao wamelazwa katika mikoa 10 na kwamba mikoa mingine 16 haijaripoti mgonjwa yeyote kufikia sasa.

Katika hotuba yake bungeni, Bw Majaliwa aliwataka Watanzania waendelee kutekeleza kanuni za idara za afya za kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Tanzania iliacha kutangaza takwimu za maambukizi Aprili wakati wagonjwa walipoanza kuongezeka kwa kasi na kufika 509. Rais Magufuli amekuwa akilaumiwa na viongozi kadhaa kimataifa kwa kutochukulia kwa uzito ugonjwa huo wa Covid-19.

Rais huyo, anayeripotiwa kukataa pia kushauriana na viongozi wenzake wa Afrika Mashariki kuhusu juhudi za pamoja za kuepusha maambukizi, husema Tanzania inaamini uwezo wa Mungu kuponya magonjwa na pia wamejaaliwa mitishamba tele iliyo na nguvu za kuponya.