Mahakama yaamuru Wachina wanne warudishwe kwao
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA Jumatano iliamuru raia wanne wa Uchina walionaswa katika video wakimchapa Mkenya warudishwe nchini kwao mara moja.
Hakimu Mwandamizi, Bi Hellen Onkwani aliamuru Deng Hailan, Ou Qiang, Yu Ling na Chang Yueping wasafirishwe mara moja kufuatia agizo la Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i.
Kiongozi wa mashtaka alimfahamisha Bi Onkwani kuwa uchunguzi alioamuru ufanywe kuwahusu washtakiwa hao umekamilika.
“Baada ya kuwasiliana na idara kadhaa za Serikali uamuzi umefikiwa washukiwa hawa warudishwe nchini Uchina,” hakimu alifahamishwa.
Mahakama ilikabidhiwa waraka uliokuwa umetiwa sahini na Waziri wa Usalama kwamba “ raia hao wa kigeni warudishwe kwao.” Kupitia kwa mkalimani washukiwa hao hawakupinga agizo warudishwe kwao.
Deng Hailan, Ou Qiang, Yu Ling na Chang Yueping wamekuwa kizuizini kufuatia agizo la Bi Onkwani mapema mwezi huu.
Kurudishwa kwa Wachina hao kunafuatia agizo wafunguliwe mashtaka.
Jaji Luka Kimaru wa mahakama kuu alikuwa ameamuru wiki iliyopita washukiwa hao wasirudishwe kwao.