Maji ya chupa yamejaa chembechembe za kinyesi – Ripoti
Na STELLAR MURUMBA
WAKENYA wanaodhani kwamba huepuka magonjwa wanapokunywa maji ya chupa huenda wamekuwa wakiweka maisha yao hatarini bila kujua.
Uchunguzi uliofanywa kwenye maabara umebainisha kuwa maji ya chupa yanayotengenezwa na kampuni mbalimbali, zikiwemo kubwa kubwa zinazoaminika kwa ubora wa bidhaa, yamejaa kemikali na uchafu ikiwemo chembechembe za kinyesi.
Maji yaliyonunuliwa kutoka kwa mitaa tofauti ya Nairobi kama vile Eastleigh, Buruburu na katikati mwa jiji yalitoa matokeo ya kushtua, kwani uchunguzi katika maabara ya serikali ulibainisha asilimia 40 ya maji hayo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Hata hivyo, uchunguzi ulioshtua zaidi ni ule uliofanyiwa maji yaliyonunuliwa Kitale katika Kaunti ya Trans Nzoia, ambapo asilimia 10 ya maji ya chupa ilipatikana kuwa na bakteria ya E-coli, ambayo hupatikana kwenye kinyesi cha binadamu au wanyama.
“Uchafu wowote unaweza kusababisha hatari kwa sababu ya jinsi maji ya chupa yanavyosambazwa maeneo mengi kwa kasi. Inahitajika pia kuwe na uchunguzi wa mara kwa mara kutambua uwepo wa bakteria kwenye maji, na lazima kampuni za kutengeneza maji haya zizingatie kanuni za hali ya juu ya usafi,” ripoti ya uchunguzi huo ikapendekeza.
Katika uchunguzi jijini Nairobi, maji mengi yalipatikana kuwa na kemikali hatari kwa kiwango cha juu ambacho kinaweza kusababisha maradhi kama vile saratani.
Ingawa kemikali ya Chlorine hukubalika kusafisha maji ya kunywa, ilipatikana kuna kampuni ambazo hutia kemikali hiyo kwa wingi kupita kiasi kinachoruhusiwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), na hivyo basi kuhatarisha maisha ya binadamu.
Hata hivyo, Msemaji wa Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Kenya (KEBS), Bi Patricia Kimanthi, alisema maji ya chupa kutoka kwa kampuni zilizoidhinishwa na KEBS yanafikia kiwango cha ubora unaohitajika. Hii ni licha ya kuwa baadhi ya kampuni hizo ni miongoni mwa zile zilizochunguzwa kwenye utafiti huu.
Katika mwaka wa 2016, KEBS liliorodhesha maji kuwa miongoni mwa bidhaa zilizo na hatari zaidi nchini kwa sababu ya ongezeko kubwa la makampuni haramu ya utengenezaji wa maji ya chupa.
Wakati huo, kulikuwa na makampuni 600 ya kutengeneza maji hayo nchini na mengine yakafungwa na serikali baada ya kupatikana kukiuka sheria za utengenezaji wa bidhaa kwa njia salama huku zingine zikiwa hazina leseni.