• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 6:17 PM
Makanisa sasa yazoea hali ya waumini kuombea nyumbani

Makanisa sasa yazoea hali ya waumini kuombea nyumbani

NA SAMMY WAWERU

Wiki ya pili, makanisa kote nchini yamesalia kufungwa kufuatia agizo la serikali ili kusaidia kudhibiti maenezi ya Covid – 19.

Mwezi uliopita, Machi 22, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aliamuru maeneo yote ya kuabudu kufungwa, kwa kile alitaja kama “kuzuia watu kukongamana”.

Ili kuzuia usambaaji zaidi wa virusi hatari vya corona, serikali pia iliagiza mabaa, maeneo yote ya burudani kufungwa, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku hafla za harusi kwa muda, huku mazishi yakitakiwa kufanywa kwa muda mfupi iwezekanavyo na kuhudhuriwa na watu wachache mno.

Awali licha ya baadhi ya maeneo ya kuabudu kukaidi amri hiyo, kwenye uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali makanisa sasa yameonekana kuitii.

Mnamo Jumapili, makanisa tuliyozuru mitaa kadhaa kaunti ya Nairobi na Kiambu, milango ilisalia kufungwa, kinyume na ilivyokuwa awali kabla visa vya maambukizi ya Covid – 19 kuripotiwa kuongezeka nchini.

Kufikia sasa, Kenya imethibitisha zaidi ya watu 170 walioambukizwa corona, huku sita wakifariki kutokana na virusi hivyo hatari.

Sawa na makanisa mengine, African Inland Church, AIC, tawi la Zimmerman, milango yake ilisalia kufungwa.

Milango ya Glory Realm International Ministries maarufu kama Kings Domain, kanisa lililoko pembezoni mwa Thika Super Highway, Clayworks Kasarani, pia lilifungwa.

Aidha, kwenye mlango wa kanisa hilo, ujumbe umechapishwa, ukiarifu: “Kufuatia amri ya serikali, kanisa limesalia kufungwa hadi serikali itakapotoa mwelekeo”.

Kibango hicho pia kimeeleza ibada inavyoendeshwa. “Ungana nasi kupitia mtandao wa Facebook na You Tube, kila Jumanne na Jumapili, tukipeperusha moja kwa moja ibada,” ujumbe huo unaarifu.

Makanisa kadhaa yamegeukia na kukumbatia mitandao ya kijamii, wahubiri na washirika wachache wakiendesha ibada; mahubiri yanayoandamana na nyimbo, yanayopeperushwa kupitia Facebook Live.

Isitoshe, nambari ya kutoa sadaka na fungu la kumi, pia inachapishwa, kwa wanaoyafuatilia. “Mhubiri wetu akimaliza kutulisha chakula cha kiroho, anatuhimiza tutoe sadaka na fungu la kumi,” akasema mshirika wa kanisa la PEFA, tawi la Kimbo Ruiru.

Mengine yanatumia vyombo vya habari, kama vile runinga na redio, kupeperusha mawimbi ya mahubiri yake moja kwa moja.

Hata hivyo, kuna baadhi wanakosoa amri ya serikali kufunga makanisa. Duncan Ndegwa Bull kwenye chapisho lake katika Facebook, “Makanisa yafunguliwe” , ameeleza kushangazwa kwake na amri hiyo, huku matatu, maduka hasa ya kijumla, na benki, yote yakiruhusiwa kuhudumu licha ya idadi kuu ya wateja wanaopokewa.

“Ni sahihi kwa watu 40 kukusanyika kwenye basi inayosafiri Mombasa hadi Kisumu, lakini ni hatia kwa watu 10 kukusanyika kanisani kuomba. Ni sawa watu 50 kuwa kwenye duka la kijumla wakinunua bidhaa ila si kanisani wakilishwa chakula cha kiroho.

“Ni sawa kwa watu 100 kuwa kwenye benki kuanzia asubuhi mpaka alasiri, lakini si mkusanyiko wa watu 10 kanisani. Kuna uhalisia upi hapo?” ameshangaa. Ndegwa ameendelea kueleza, akitoa mfano wa kanisa analohudhuria akitaja lina takriban washirika 300, kabla ya amri ya serikali liliendesha ibada ya watu wasiozidi 30, kwa makundi kila saa moja na kuzingatia umbali wa mita mbili baina ya mtu na mwingine.

“Wote walirejea makwao wakiwa wamefurahi kwa takaso la chakula cha kiroho. Kwa nini utaratibu huo usitekelezwe, kila kanisa lipewe idadi? Kufunga makanisa si suluhu ila ni kubuni shida kubwa kuliko janga la Covid – 19. Makanisa yafunguliwe,” Ndegwa anaeleza.

Kuna wanaopinga pendekezo hilo, James Mutindi, akihoji kanisa ni roho ya mtu binafsi ila si jengo. “Sikubaliani na pendekezo la aina hiyo, tuoneshe washirika kuwa Mungu yu hai ndani yao, ila si kwenye makanisa,” Mutindi akachangia.

“Ni kina nani watahudhuria na ni kina nani watakosa, ili kuzingatia umbali baina? Inaonekana Wakenya hawajaona athari za huu ugonjwa. Wasiofuata amri na maagizo ya serikali watakuja kujuta siku moja,” Salome Gitonga Wa Phq ameonya.

Serikali imeshikilia haiturusu watu kukongamana kwa vyovyote vile, ikisema virusi hatari vya corona sasa vinasambaa miongoni mwa watu, ndani kwa ndani hapa nchini. Mataifa ya Marekani, Italia, na Uhispania, yameonekana kulemewa na janga la Covid – 19, kutokana na takwimu za waliofariki kupitia ugonjwa huo na maambukizi zaidi.

You can share this post!

Afueni baada ya masoko Githurai kufunguliwa

Mwandishi wa Pakistan achapisha kitabu kuhusu Mkenya mpenda...

adminleo