Habari Mseto

Makanisa yatishia kupinga BBI

November 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na Valentine Obara

VIONGOZI wa makanisa ya kievanjelisti nchini, wameapa kufanya kampeni za kupinga mabadiliko ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), ikiwa ripoti iliyotolewa haitafanyiwa marekebisho.

Katika kikao cha wanahabari Nairobi, viongozi hao walisema ingawa kuna mambo mazuri wanayokubaliana nayo kwenye ripoti hiyo, maoni yao hayakujumuishwa.

Wakiongozwa na Askofu Mark Kariuki wa Kanisa la Deliverance, walisema hali ya sasa ambapo baadhi ya viongozi wamesisitiza hakuna marekebisho yatafanywa, ni sawa na ilivyokuwa 2010 ambapo mgawanyiko uliendelea kushuhudiwa licha ya kupitishwa kwa katiba mpya.

“Tusiache yeyote nje kama kwamba tunamrekebishia mtu mmoja katiba. Kwa maoni yangu kibinafsi, hata kama itabidi kuongeza muda wa serikali iliyo mamlakani ndipo tupate muda wa kujadiliana kuhusu BBI, heri tufanye hivyo ili tudumishe umoja wa nchi,” alisema.

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga amesisitiza hakuna marekebisho yatafanyiwa ripoti ya BBI tena.