Habari Mseto

Makueni yaahidiwa maji safi kutoka Mzima Springs

September 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PIUS MAUNDU

SERIKALI inapanga kusambaza maji kutoka chemchemi ya Mzima hadi Kaunti ya Makueni, kwa mujibu wa Waziri wa Maji, Bw Simon Chelugui.

Waziri alisema kufuatia ombi la viongozi wa Makueni, wizara ilifanikiwa kupanua usambazaji maji ya Mzima hadi kwa kaunti hiyo.

Hili litafanikishwa wakati wa mpango wa Mzima 2, ambao umenuiwa kusambaza maji zaidi kwa kaunti za Mombasa na kaunti nyingine za Pwani.

“Tuna imani kwamba wakati mradi wa Mzima 2 utakapoanza Juni mwaka ujao, kutakuwa piai na sehemu ya kufikisha maji Mtito Andei, Machinery na Kibwezi,” akasema Bw Chelugui.

Alikuwa akizungumza katika kijiji cha Kivuthini, Kaunti ya Makueni wakati wa mazishi ya Mzee Pius Maingi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mazishi hayo yalihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mafuta Kenya, Hudson Adambi, Waziri wa Maji Makueni, Robert Kisyula na Mbunge wa Kibwezi mashariki, Jessica Mbalu.

Tangazo hilo lilitolewa wakati ambapo eneo hilo lingali linakumbwa na ukame mkali.

Inatarajiwa mradi huo utachangia pakubwa kupunguza matatizo ya maji Makueni, kwani pia serikali ya kaunti inajitahidi kuanza kusambaza maji kutoka kwa chemchemi hiyo iliyo katika mbuga ya wanyama ya Tsavo Magharibi.

Wakati huo huo, waziri alitangaza serikali inaendeleza juhudi za kuanzisha mradi wa usambazaji maji wa Sh250 milioni katika kaunti hiyo kuboresha hali mjini Wote, ambako ni makao makuu ya serikali ya kaunti.

Mamia ya wakazi mjini humo hutatizika kupata maji safi baada ya kisima cha Kamunyolo walichokuwa wakitegemea, kuharibika baada ya mafuriko mwaka uliopita.