Makundi ya 'Tangatanga' na 'Kieleweke' yamchanganya Sonko
Na LEONARD ONYANGO
MGAWANYIKO ndani ya chama cha Jubilee umemwacha Gavana wa Nairobi Mike Sonko katika njiapanda kisiasa.
Gavana huyo ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto, hata hivyo, anashikilia kuwa haungi mkono makundi yote mawili; ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’, ambayo yamechipuka katika chama cha Jubilee.
Kundi la Tangatanga linaunga mkono Dkt Ruto kuwania urais katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa 2022 huku Kieleweke wakimpinga.
Wiki mbili zilizopita, Bw Sonko aliwashambulia hadharani aliyekuwa mwaniaji wa ugavana wa Nairobi Peter Kenneth na mbunge Maalumu Maina Kamanda huku akiwataja kuwa wafisadi mbele ya waumini wa kanisa la St Stephens ACK Nairobi.
Bw Kenneth na Bw Kamanda ni miongoni mwa wanasiasa wa kundi la Kieleweke linalopinga vikali Naibu wa Rais Dkt Ruto kuwania urais 2022.
Bw Kamanda ni miongoni mwa wanasiasa kutoka eneo la Kati waliopoteza kura za mchujo za Jubilee kabla ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017 na wamekuwa wakishutumu Dkt Ruto kwa ‘kuwaangusha’.
Katika hotuba yake kanisani, Bw Sonko pia alishambulia kundi la Nairobi Regeneration, lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta kusafisha na kupangilia upya jiji la Nairobi.
Bw Sonko alisitisha shughuli ya kubomoa vibanda na majumba yaliyojengwa katika hifadhi ya barabara au eneo la serikali hadi pale atakaposhauriana na rais.Sonko na Waziri wa Utalii Najib Balala ndio wenyeviti wa kamati ya Nairobi Regenaration.
Bw Sonko pia alikosoa Rais Kenyatta kwa kuwatoza wafanyakazi ada ya asilimia 1.5 ya mishahara kwa ajili ya Mpango wa Ujenzi wa Nyumba nafuu.
“Naunga mkono mradi wa ujenzi wa nyumba nafuu na miradi minne mikuu ya rais wetu mpendwa ambaye ni rafiki na ndugu yangu mkubwa. Mpango huo utawezesha Nairobi kupata nyumba 200,000 ndani ya kupindi cha miaka mitatu. Lakini napinga hatua ya Rais kutaka kuwatwika mzigo mkubwa wa kulipa ada wakazi wa Nairobi na Wakenya wote kwa ujumla,” akasema Bw Sonko.
Rais Kenyatta amekuwa akitetea ada hiyo akisema kuwa mpango huo utawezesha Wakenya wasioweza kumudu bei ya juu ya nyumba kujipatia makazi.Naibu wa Rais Dkt Ruto, hata hivyo, hajajitokeza wazi na kutangaza msimamo ikiwa anaunga mkono ada hiyo ya asilimia 1.5 au la.
Mapema 2018, Gavana Sonko alidai kuwa baadhi ya mabwanyenye kutoka eneo la Mlima Kenya walikuwa wakifanya vikao vya usiku kupanga njama ya kumzuia Dkt Ruto kuwa rais 2022.
Bw Sonko aliapa kukabiliana na yeyote ambaye angethubutu kumzuia Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta.Ilikuwa baada ya matamshi hayo ambapo alijipata pabaya na Ikulu na kupunguziwa walinzi kutoka 26 hadi watano.
Bw Sonko aligura Nairobi na kwenda kusihi nyumbani kwake katika Kaunti ya Machakos akidai kuwa maisha yake yalikuwa hatarini.
Gavana Sonko pia amekuwa akishutumu baadhi ya watu katika afisi ya rais kwa kumlazimisha kuteua mtu fulani kuwa naibu wake.Bw Sonko amekuwa akihudumu bila kuwa na naibu gavana tangu kujiuzulu kwa Polycarp Igathe mwaka mmoja uliopita.
Mwaka wa ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga pia unaonekana kumkanganya zaidi Bw Sonko.Bw Sonko wiki mbili zilizopita aliambia Kamati ya Seneti kwamba amechelewa kuteua naibu wake kwa sababu alipokea ombi kutoka kwa chama cha ODM kikimtaka kuteua Bi Rahab Wangui.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Bw Sonko amekuwa akiungwa mkono na Dkt Ruto hata wakati wa kura za mchujo wa chama cha Jubilee.
“Viongozi wakuu serikalini waliunga mkono Bw Peter Kenneth, lakini Dkt Ruto alisimama na Bw Sonko. Hivyo ni rahisi kwa Sonko kuegemea Tanga Tanga kuliko Kieleweke,” anasema Bw George Mboya, mdadisi wa masuala ya kisiasa.