Maraga ateua jopo kusikiza kesi ya kuvunja Bunge
Na JOSEPH WANGUI
JAJI Mkuu David Maraga amebuni jopo la majaji watano ambao watasikiza na kuamua kesi zilizowasilishwa mahakamani kuhusiana na ushauri aliotoa kwa Rais Uhuru Kenyatta kuvunja Bunge la Kitaifa.
Bw Maraga alitoa ushauri huo Septemba 21, akisema kuwa bunge linapaswa kuvunjwa kwa kukosa kupitisha sheria kuhusu usawa wa jinsia.
Jopo hilo litaongozwa na Jaji Lydia Achode. Wengine waliojumuishwa ni George Odunga, James Makau, Anthony Ndung’u na Pauline Nyamweya.
Kubuniwa kwa jopo hilo ni kufuatia maagizo yaliyotolewa na Jaji Weldon Korir.
Walalamishi wanataka ushauri huo kuzingatiwa.
Wale wanaotaka ushauri huo kufutiliwa mbali ni Bunge la Kitaifa, wakili Kamotho Njenga, wapigakura wawili na Mbunge wa Mathare, Anthony Oluoch.
Kwenye malalamishi yake aliyowasilisha wiki iliyopita, Bw Oluoch alisema kuwa Jaji Maraga alivunja haki za kisiasa za wabunge.
Vile vile, alisema Bw Maraga alikiuka haki ya kisheria ya wabunge kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitano.
Mbunge huyo pia alisema Bw Maraga alikosea kisheria, kwani hakuzishirikisha taasisi zingine alipotoa ushauri huo, kama inavyohitajika kisheria.
Bw Oluoch alisema Jaji Mkuu angewaarifu wabunge kwanza sababu ya kuchukua uamuzi huo kabla ya kumshauri Rais Kenyatta, kwani ndio waathiriwa wakuu wa ushauri huo.
Aliiomba mahakama kutoupendelea upande wowote, kwani si Bunge pekee linalopaswa kutekeleza sheria hiyo.
“Si wabunge pekee wanaopaswa kulaumiwa kwa usawa wa kijinsia kutofikiwa kwenye Bunge la Kitaifa na Seneti,” akasema.
Alieleza kwamba kwa mujibu wa vipengele 38(2)(a) na 38(3)(b) vya Katiba, Wakenya wako huru kuwachagua viongozi wanaowataka bila mwingilio wowote.
Chaguzi huwa zinaendeshwa nchini katika hali ambapo wapigakura hutekeleza haki yao kuwachagua viongozi wanaowataka kwa njia ya siri.
Katika hali hiyo, alisema kuwa kando na wabunge maalum, wabunge wengine walichaguliwa na wananchi kwa njia huru.
“Wapigakura huwa hawahitajiki kuzingatia sheria hiyo wanapofanya maamuzi kuhusu viongozi watakaowaongoza. Hawawajibiki ikiwa viongozi watakaowachagua Bungeni watatimiza mahitaji ya sheria hiyo kwa msingi wa vipengele 97 na 98 vya Katiba au la,” akasema Bw Oluoch.
Vivyo hivyo, alisema Bunge na wabunge hawana hitaji lolote kisheria kuzingatia sheria hiyo.
Aliongeza kuwa kijumla, ushauri huo haufai kwani kuna miswada mingine ya kuibadilisha katiba na kesi kadhaa ambazo ziko mahakamani kuhusiana na utekelezaji wa sheria hiyo.