Habari Mseto

Maseneta waitaka serikali kurejesha leseni za kampuni za kamari zilizozimwa

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wameitaka serikali kuziruhusu kampuni za kamari na ubashiri ambazo leseni zao zilifutiliwa mbali kuendelea na shughuli zao huku suala la iwapo zimekuwa zikilipa ushuru au la likishughulikiwa na wadau katika sekta hiyo.

Wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Sheria na Masuala ya Haki ya Kibinadamu Jumatano waliisuta Bodi ya Kudhibiti Michezo ya Kamari na Bahati Nasibu (BCLB) kwa kudharau agizo la mahakama lililositisha hatua hiyo dhidi ya kampuni 27 za kamari.

“Hatua hiyo ilichukuliwa kabla ya kutatuliwa kwa mzozo kuhusu ushuru ambao uko mbele ya Jopo la Kutatua Mizozo kuhusu Ushuru (TAT). Huu ni ukiukaji wa sheria na haki za kampuni husika ambazo zinawaajiri Wakenya wengi hasa vijana,” amesema mwenyekiti wa kamati hiyo Samson Cherargei.

Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Masuala ya Sheria na Haki, Samson Cherargei akizungumza na Waziri Msaidizi wa Fedha Nelson Gaichuhie na Maseneta wengine baada ya kukutana na wakuu wa baadhi ya kampuni za kamari zilizonyimwa leseni mpya. Hapa ni katika ukumbi wa County, ambako Kamati hiyo ilikutana na wadau hao kusikiliza malalamishi kuhusu suala hilo. Picha/ Charles Wasonga

Amesema hayo Jumatano wakati wanachama wa kamati hiyo wamekutana na wakuu wa kampuni nne za kamari miongoni mwa 27 zilizozimwa kusikia malalamishi yao. Kampuni hizo ni; Sportspesa, Betin, Betways, na BetPewa.

Waziri Msaidizi wa Fedha Nelson Gaichuhie na Kamishna wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) Bi Elizabeth Meyo wamehudhuria mkutano huo kuwakilisha serikali.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na kaimu Mkurugenzi Mkuu wa bodi ya BCLB Liti Wambua hawakuhudhuria licha ya kupata mwaliko wa kamati hiyo.

Akitetea KRA Bi Meyo amesema habari zinaonyesha kampuni husika za kamari hazijalipa malimbikizi ya ushuru ya kima cha Sh61 bilioni.

“Kiasi kikuu cha cha fedha hizo ni ushuru kutokana na pesa ambazo wacheza kamari hushinda. Ushuru huu ulianzishwa mwaka 2018 kupitia Mswada wa Fedha wa 2018,” akasema.

Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya SportsPesa Ronald Karauri ametilia shaka kiwango hicho cha fedha akisema kampuni yake ilitozwa ushuru wa juu kuliko inavyohitajika.

“Ikiwa tumelipa jumla ya Sh17 bilioni kama ushuru kwa miaka mitano tangu tulipoanza shughuli zetu humu nchini, mbona KRA sasa inadai kuwa tunapaswa kulipa ushuru wa Sh22 bilioni kwa mwaka mmoja. Kuna kasoro hapa na ndio maana tuliwasilisha malalamishi yetu kwa jopo la TAT,” amesema Karauri.

Akaongeza: “Lakini hata kabla ya malalamishi yetu kushughulikia bodi ya BCLB iliamuru leseni yetu ifutuliwe mbali. Tuliona huu ulikuwa ukiukaji wa haki zetu na ndipo tukawasilisha kesi mahakamani.”