Masikitiko wakulima wa pamba kuvuna hewa
NA KALUME KAZUNGU
WAKULIMA wapatao 10,000 wa zao la pamba tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu wanakadiria hasara kufuatia mmea huo kuvamiwa na wadudu aina ya Red Spider.
Wakulima hao kutoka vijiji vinavyokuza pamba kwa wingi, ikiwemo Baharini,Uziwa, Tewe na Nairobi Area walisema hawatavuna chochote mwaka huu kutokana na uharibifu unaoendelezwa na mdudu huyo.
Msemaji wa wakulima wa pamba, Kaunti ya Lamu Joseph Migwi, aliambia Taifa Leo Jumanne kwamba zaidi ya ekari 10,000 za pamba zimeharibiwa na Red Spider Mite hasa baada ya juhudi za wakulima kuwanyunyizia dawa wadudu hao kugonga mwamba.
“Mwaka huu hatutaweza kuvuna chochote. Pamba yetu imeharibiwa kabisa na wadudu aina ya Red Spider Mite. Wadudu hao wamekuwa wakiharibu maua ambayo tulitarajia yangezalisha pamba. Tumeambulia patupu,” akasema Bw Migwi.
Baadhi ya wakulima waliozungumza na Taifa Leo walieleza hofu kwamba kukosekana kwa zao hilo mwaka huu huenda kukachangia wanafunzi kufukuzwa shuleni kutokana na ukosefu wa karo.
Bw Peter Kariuki ambaye ni mmoja wa wakulima wa pamba eneo la Mpeketoni alisema kwa miaka mingi amekuwa akitegemea kilimo cha pamba ili kukimu mahitaji ya familia yake, ikiwemo ulipaji wa karo kwa wanafunzi.
“Hatuna mavuno yoyote mwaka huu. Tegemeo langu kuu lilikuwa ni hiyo pamba. Sielewi nitalipa vipi karo ya watoto wangu hasa baada ya pamba yote kuharibiwa na wadudu,” akasema Bw Kariuki.
Wakulima sasa wanaitaka serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuingilia kati na kuwasaidia kukabiliana na wadudu hao waharibifu.
Wakulima hao pia waliiomba serikali kuwatafutia soko la jumla la zao hilo siku za usoni.
Wakulima walilalamika kuwa mara nyingi wamelazimika kuuza pamba yao kwa bei duni kufuatia ukosefu wa soko maalum.
Mbali na tarafa ya Mpeketoni, pamba pia hupandwa kwenye baadhi ya maeneo ya tarafa za Witu na Faza.