Matiang’i aahirisha ziara yake Keroka kwa kugongana na ya Ruto
Na CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i ameahirisha ziara yake katika eneo la Keroka, Kaunti ya Nyamira Ijumaa baada ya kubaini kuwa Naibu Rais Dkt William Ruto atakuwa akizuru eneo hilo siku hiyo.
Katika ziara yake, Dkt Ruto anasemekna kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo kando na kuhudhuria mikutano kadhaa ya kuchanga pesa kwa ajili ya kusaidia makanisa.
Dkt Matiang’i alikuwa amepangiwa kufungua rasmi jengo jipya katika Kituo cha Polisi cha Keroka, kama mgeni mheshimiwa.
Naye Dkt Ruto anaongoza ufunguzi wa afisi za Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (CDF) katika eneo bunge la Mugirango Magharibi. Baadaye siku hiyo anaweka jiwa la msingi katika mradi wa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Nyaigesa.
Naibu Rais pia ataongoza mkutano wa kuchanga pesa katika Kanisa Katoliki la Nyamira na makanisa mengine 20 ya Kiadventisti.
Isitoshe, Dkt Ruto pia ataongoza harambee kwa ajili ya kuwasaidia makundi ya akina mama katika eneo bunge la Mugirango Kaskazini.
Ziara ya Naibu Rais eneo hilo linajiri wiki moja baada ya ziara ya kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kaunti jirani ya Kisii ambapo alimtetea Waziri Matiang’I dhidi ya tuhuma kwamba alihusika katika sakata ya dhahabu feki.
Akiwahutubia waombolezaji katika eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini Bw Odinga alidai kuwa Dkt Matiang’i ni “mweupe kama pamba” huku wakiwasuta wanaoingiza jina lake katika sakata hiyo kama watu ambao hawapendezwi na kazi nzuri anayotekeleza.
“Ningependa kuwaambia wale ambao wanadai Dkt Matiang’I anahusika katika sakata hiyo wahamu kuwa huyu ni mtumishi wa umma mwadilifu mno. Yeye ni mweupe kama pamba. Nimefanya naye kazi zamani nikiwa Waziri Mkuu na utendakazi wake ulikuwa wa kupendeza mno,” akasema Bw Odinga.
Ziara ya Dkt Ruto eneo hilo pia inajiri siku chache baada ya Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Richard Onyonka kutangaza kuwa amegura vuguvugu la Tangatanga.