Habari Mseto

Mbunge apuuza EACC, asema alikopeshwa hela zinazodaiwa kuwa hongo

Na HILARY KIMUYU August 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Kimilili Didmus Barasa amekanusha madai kwamba amewahi kula rushwa kutoka kwa mtu yeyote.

Alisema haya alipoagizwa kufika mbele ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusu madai ya kuitisha hongo ya Sh2 milioni kutoka kwa mwanamke mfanyabiashara mwaka uliopita, 2023.

Alisema Jumapili, Agosti 25, 2024 kuwa pesa hizo zilikuwa mkopo kutoka kwa mwanasiasa huyo.

Bw Barasa alisema mwanasiasa huyo aliyewahi kugombea ugavana ndiye chanzo cha masaibu yake ambapo baada ya kutofautiana naye kuhusu malipo ya deni hilo, alizua madai hayo ya rushwa ili kumpaka tope.

“Ningependa kukufahamisha kuwa Sh2, 000, 000 zilizotumwa kwenye akaunti yangu ya benki zilikuwa mkopo kutoka kwa mwanasiasa huyo aliyewania bila kufua dafu ugavana katika kaunti moja nchini, Desemba 13, 2023. Nakala hizo zinafanana kabisa na zinazotumika katika mchakato wa kutuma pesa katika akaunti ya benki, zinaashiria ni mkopo, unaweza kuzidurusu. Suala kuhusu ni kwa nini sijalipa, ikiwemo mvutano kuhusu masharti ya kandarasi si tatizo lenu,” alisema Bw Barasa.

Alisema suala hilo liliripotiwa kwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) Karen na likapuuziliwa mbali.

“Hii ni kuwafahamisha kuwa sitatimiza maagizo hayo kwa sababu ni ukiukaji wa majukumu ya tume. Hamuwezi mkanialika nitawatafsirie sababu ni kwa nini hela hizo zilitumwa ilhali mmesoma nakala zinazothibitisha mchakato huo kwa sababu, hata kama kiasi kilichotumwa ni Sh100, unahitaji nakala za kuthibitisha,” alisema.

“Kama sijazingatia wajibu wa kifedha, ni kwa sababu ya mzozo kati yangu na mhusika. Ni sharti nieleze EACC kuwa mna jukumu muhimu kwa Katiba yetu. Hamna wajibu wa kusaidia mhusika kulipwa hela alizonikopesha. Mna stakabadhi zinazoonyesha ni kwa nini fedha hizo zilitumwa kwenye akaunti yangu. Acha mhusika aende kortini tukutane huko.”

Jumapili, EACC ilimwagiza Bw Barasa kujibu kuhusu madai hayo ya ulaji rushwa.

Kupitia barua iliyoandikwa Agosti 21, 2024 EACC ilisema “pesa hizo zilitumwa Desemba 13, 2023.”

Kulingana na tume, hii ni mara ya pili inamwagiza Bw Barasa kujiwasilisha kwake baada ya kukaidi kujitokeza Agosti 14, 2024 jinsi alivyoagizwa.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo