Mbunge atisha kuchochea wakazi kuua wanyamapori wanaowavamia
Na CHARLES WASONGA
MBUNGE wa Mwatate Andrew Mwadime ameonya kuwa huenda akachochea wakazi wa eneo bunge lake kuwashambulia wanyamapori wanavamia makazi yao ikiwa serikali haitadhibiti wanyama hao.
Akiongea na wanahabari Jumatano katika majengo ya bunge, Mbunge huyo alilalamika kuwa wiki hii Simba wamekuwa wakivamia mifugo wa wakazi lakini Shirika la Wanyama Pori Nchini (KWS) haijachukua hatua yoyote.
“Jumanne mama mmoja kutoka kijiji cha Kegwa aliwapoteza ng’ombe wake saba ambao walivamiwa na Simba ambao hutoka katika mbunge la wanyama la Tsavo. Kando na hayo wanyama wengine kama vile ndovu wamekuwa wakiharibu mashamba ya watu wangu na serikali haifanyi chochote,” akalalama.
Akaongeza: “Hata Katiba inamruhusu mja kujikinga ikiwa anakabiliwa na hatari. Ikiwa KWS itafeli kuwadhibiti wanyama basi hivi karibuni huenda sisi kama viongozi tukawashauri watu wetu kuchukua sheria mikononi kwa kuwashambulia wanyama hao.”
Bw Mwadime alisema Jumanne alijaribu kumfikia, kwa njia ya simu, waziri wa Utalii na Wanyama Pori Najib Balala kulalamikia kero hilo lakini hakumpata.
Vile vile, alisema amejaribu kuwasilisha malalamishi yake kwa wakuu wa KWS katika kaunti ya Taita Taveta lakini mpaka Jumatano hawakuwa wamechukua hatua yoyote kwani bado simba walikuwa wakiua mifugo wa wakazi.
“Nashangaa ni kwa nini KWS imefeli kudhibiti wanyama pori katika kaunti yetu ya Taita Taveta jinsi wanavyofanya katika kaunti ya Laikipia. Mbona faru za Laikipia zinaangaziwa,” akalalamika Bw Mwadime.
Mbunge huyo alisema kuwa inakera hata zaidi kwamba wakazi ambao mifugo wao wameuawa na wanyamapori katika eneo bunge lake la Mwatate hawajalipwa fidia kwa muda wa miaka kadhaa zilizopita.
“Ni kinaya kwamba mimi ni mmoja wa wabunge waliotunga sheria kuhusu ulipaji fidia kwa wakazi walioathiriwa na wanyama pori lakini watu wangu hawajalipwa tangu sheria hiyo ilipoanza kufanyakazi,” Bw Mwadime akalalamika.
Kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita, zaidi ya mifugo 300 wameuawa na Simba pamoja na wanyama wengine ambao huvamia makazi hata nyakati za mchana.
Bw Mwadime alisema wiki jana, mwanamke mmoja aliyepoteza ng’ombe saba alisema kama angalikuwa na mkuki angewashambulio Simba hao bila kujali mkono wa sheria.