MCK yataka visa vya wanahabari kuvamiwa vichunguzwe
Na BENSON MATHEKA
OFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) inafaa kuchunguza visa vya kushambulia wanahabari wakiwa kazini na kuharibu vyombo vyao, Baraza la Wanahabari Kenya (MCK) limesema.
Baraza hilo liliungana na Chama cha Wanasheria nchini (LSK) na Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu (KNHRC) kushutumu kisa cha Jumatatu usiku ambapo polisi waliwashambulia wanahabari waliokuwa wakinasa na kupeperusha habari za kuwasili nchini kwa wakili Miguna Miguna.
“KNHRC, LSK na MCK tunachukulia vitendo vya hivi majuzi vya polisi kama unyanyasaji wa wanahabari wakiwa kazini.Tunataka kufahamisha serikali na hasa polisi kwamba wanahabari hao wana vibali rasmi na wanaongozwa na mwongozo wa maadili ya uanahabari unaotekelezwa na Baraza la Wanahabari la Kenya,” ilisema taarifa ya pamoja ya mashirika hayo.
Mwanahabari wa runinga ya Citizen Stephen Letoo, Robert Gichira wa runinga ya NTV na Sofia Wanuna wa KTN walinyanyaswa na kupigwa na maafisa wa polisi katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Stephen Letoo na Gichira walijeruhiwa na vyombo vyao kuharibiwa.
KNHRC, LSK na MCK tunasema kuwa vinatambua mazingira magumu ambayo wanahabari wanahudumu katika juhudi za kukusanya habari.
“KNCHR, LSK na MCK tunalaani vikali kunyanyaswa kwa wanahabari na kuchukulia kisa hiki kama tisho kwa usalama wao,” ilisema taarifa yao.
“Tuna imani kwamba Mamlaka Huru ya kuchunguza utendakazi wa polisi (Ipoa) itachunguza kwa kina kisa cha kushambulia wanahabari na watakaopatikana kuwa walivunja sheria watachukuliwa hatua.
Pia, tunaomba DPP na ofisi ya kupokea malalamishi ya umma kuchunguza kisa hiki na kuwachukulia hatua waliohusika,” taarifa hiyo ilisema.