Mkenya atupwa ndani maisha China kwa kulangua kokeini
Na AGGREY MUTAMBO
MAHAKAMA ya China imemhukumu Mkenya kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la ulanguzi wa dawa za kulevya.
Kesi hiyo imefichua mbinu hatari wanazotumia walanguzi wa mihadarati kusafirisha bidhaa hiyo haramu.
Simon Wambua Mbuvi, 44, alihukumiwa kifungo cha maisha na mahakama ya Guangzhou iliyoko mkoani Guangdong wiki mbili zilizopita, na sasa atajiunga na Wakenya wengine zaidi ya 30 wanaozuiliwa China kutokana na ulanguzi wa mihadarati.
Stakabadhi za kortini zilizoonwa na Taifa Leo, zinaonyesha kuwa Jaji Hu Peng na wenzake Wen Fangdao na Huang Jian walimpata Mbuvi na hatia ya kubeba gramu 947 za kokeini tumboni.
Mbuvi angehukumiwa adhabu ya kifo endapo angepatikana na kilo moja au zaidi ya mihadarati, kulingana na sheria ya China.
Mbuvi ambaye jina lake limerekodiwa kama ‘Mbuwe’ katika stakabadhi za korti ya China alikamatwa mnamo Novemba 23, mwaka jana mara tu baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Guangzhou kwa kutumia ndege ya Ethiopia, ET616.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Mkenya huyo kuzuru China na alifaa kurejea nchini Kenya Desemba 3, 2018 baada ya kufikisha ‘mzigo’.
Kabla ya kuondoka humu nchini, mwanamke aliyejulikana kwa jina la Breda alimwendea Mbuvi, aliyekuwa akifanya kazi ya shambani, na kumwahidi kitita cha Sh205,000 endapo angemfanyia kazi fulani.
Breda ambaye pia alifahamika kama Fridah, alinunulia Mbuvi tiketi za ndege na kulipia viza na kumtambulisha kwa wakuu wa mtandao wa ulanguzi wa mihadarati. Breda, hata hivyo, hakumweleza Mbuvi kuwa alikuwa anaenda kusafirisha dawa za kulevya.
Mnamo Novemba 24, Mbuvi alianza safari ya kuelekea nchini China kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Aliwasili Addis Ababa, Ethiopia saa mbili baada ya kuondoka JKIA. Akiwa Addis Ababa alipokelewa na watu wawili.
Alipokuwa akisubiri ndege ya kuelekea Guangzhou mnamo Novemba 24, wanaume hao wawili walimpa chakula na wakamwambia apumzike.
Baadaye, walimpa tembe 79 baada ya kumwonyesha namna ya kumeza tembe moja baada ya nyingine kwa kutumia maji na soda. Alipowauliza kwa nini alikuwa anameza tembe walimwambia alihitaji kuwa na joto anaposafiri hewani kwa muda mrefu.
Baadaye, saa 12 jioni walimpeleka katika uwanja wa ndege ambapo aliabiri ndege na kuelekea nchini China.
Alipewa maagizo kwamba asile kitu chochote ndani ya ndege hata baada ya kusafiri kwa muda wa saa 12.
Kulikuwa na maajenti wa mtandao wa ulanguzi wa mihadarati waliokuwa wakimsubiri nchini China ambao wangempokea na kuhakikisha kuwa wanachukua kinyesi chake na kutoa tembe alizokuwa amemeza.
Uhamiaji
Lakini alipotua nchini China, maafisa wa idara ya uhamiaji walimnasa baada ya mashine za X-ray kumpata na vitu visivyo vya kawaida tumboni.
Mbuvi alifikishwa mahakamani ambapo alikanusha mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya. Lakini alijipata pabaya siku mbili baadaye alipoenda haja na kinyesi chake kupatikana na tembe 79 za kokeini.
Uchunguzi uliofanywa katika hospitali ya kijeshi ya mkoa wa Guangdong ulibaini kuwa Mbuvi hakuwa akitumia dawa za kulevya.
Mbuvi, kupitia kwa mkalimani, aliambia korti kwamba hakujua kwamba alimeza vidonge vya dawa za kulevya.
“Nilikutana na rafiki yangu wa kike akanipa fedha nimfanyie kazi ambayo sikuambiwa kwamba ilikuwa kusafirisha dawa za kulevya. Niko na namba yake ya simu na simfahamu vyema,” Mbuvi akaambia mahakama.
Lakini mahakama ilishikilia kuwa alikuwa amebeba dawa ambazo ni hatari kwa jamii.
Upande wa mashtaka uliwasilisha arafa za Whatsapp ambapo Mbuvi alikuwa akiwasiliana na wakuu wa mtandao wa mihadarati nchini Kenya na China.
Serikali ya China ilitwaa paspoti yake AK0151830 ambayo itarejeshwa kwa serikali ya Kenya.