• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Moto waharibu mali yenye thamani kubwa katika duka la magodoro Mombasa

Moto waharibu mali yenye thamani kubwa katika duka la magodoro Mombasa

Na MISHI GONGO

MALI yenye thamani kubwa imeteketea mjini Mombasa baada ya moto kuzuka katika duka la kuuza magodoro na vitambaa.

Duka hilo ni miongoni mwa maduka mengine matatu katika jumba la ghorofa tatu eneo la Sabasaba ambayo yameteketea.

Moshi mkubwa mweusi umetanda eneo hilo na kufanya kuona kuwa vigumu.

Kulingana na mkuu wa kitengo cha zimamoto katika Kaunti ya Mombasa Bw Swaleh Mwamlevi, moto huo ulioanza saa tano asubuhi ulisababishwa na cheche kutoka kwa mashine ya kuchomelea (welding machine) na ambazo ziliruka na kushika vitambaa kabla ya kusambaa.

“Wamiliki wa duka hilo walikuwa wanachomelea wakati biashara inaendelea. Ni cheche hizo zilizosababisha moto,” amesema Bw Mwamlevi.

Ameongeza kwamba waliarifiwa kuhusu mkasa huo mwendo wa saa tano na dakika ishirini (11.20a.m.) asubuhi na baada ya dakika tano walikuwa wamewasili eneo hilo.

“Tulifika chini  ya muda wa dakika tano na kufaulu kuzima moto baada ya nusu saa,” ameeleza.

Aidha Bw Mwamlevi amesema walileta magari mawili ya zimamoto ili kuudhibiti moto huo bila kuishiwa na maji.

Amesema hakuna aliyefariki au kujeruhiwa katika mkasa huo.

 

Moshi wahanikiza katika duka la magodoro na vitambaa Januari 7, 2020, mjini Mombasa. Picha/ Mishi Gongo

Mkazi katika eneo hilo Bw John Walele ameiomba Kaunti ya Mombasa kufanya mikakati kuhakikisha kuwa nyumba zote za zamani zinafanyiwa ukarabati wa nyaya za stima.

Amesema kwa sasa wakazi wana vyombo vinavyotumia umeme zaidi kuliko vile vya zamani.

“Visa vingi vya moto husababishwa na stima. Kuna nyumba zilizowekwa stima tangu miaka ya tisini (1990s) lakini sasa hivi haziwezi kudhibiti vyombo vya kielekroniki vinavyotumika kwa sasa,” akasema Bw Walele.

You can share this post!

Kenya nambari tatu ulimwenguni nchi zenye idadi kubwa ya...

Afisa wa polisi na mwanafunzi washtakiwa kwa wizi wa pombe

adminleo