Mradi wa takataka mtoni wasimamishwa
Na MWANGI MUIRURI
MBUNGE wa Maragua Bi Mary wa Maua Alhamisi alipata agizo la mahakama kuhusu mashamba na mazingira kusimamisha mradi wa takataka kujengwa kando na mto unaotumika na familia zaidi ya 30, 000.
Ilani hiyo sasa itakabidhiwa LKampuni ya Murang’a Kusini ya huduma za maji (Muswasco), kitengo cha mazingira cha serikali ya Kaunti ya Murang’a, Wizara za kitaifa kuhusu Maji na Mazingira ili kutekeleza agizo la kusimamisha mradi huo.
Akihutubia wenyeji katika eneo la mradi huo, Bi Wa Maua aliteta kuwa “mradi huu wa Sh11 Milioni unalenga kukusanya kinyesi chote cha vyoo vya miji ya Kenol, Maragua na Sabasaba na viunga husika na kukitupa hapa ambapo ni futi 10 tu kutoka mto wa Sabasaba ambao huchotwa maji ya matumizi ya kinyumbani na zaidi ya familia 30, 000 za Kaunti ya Murang’a, Machakos na Kirinyaga bila kusahau viumbe wengine wengi wanaoishi ndani ya mto huu.”
Alisema kuwa kando na mradi huo ndiko kuna mfereji mkuu wa kusambaza maji hadi Shule ya Upili ya Kamahuha na ambayo huwa na jumuia ya watu 1,500 kama wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine.
Aidha, ombi lake la kutaka mradi huo usimamishwe linaelezea kuwa kampuni ya Geoms Technologies imekiuka masharti ya utaratibu wa maadili.
“Ni mradi ambao unatekelezwa katika shamba la kibinafsi na ambapo hakuna fidia imelipwa mwenyewe. Pia, ni mradi ambao kwa sasa uko katika awamu ya asilimia 60 lakini ukiwa haujawahi kuidhinishwa na mamlaka zote husika,” akasema.
Alisema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Machi 2020 lakini Serikali kuu baada ya tetesi kuwasilishwa, ikausimamisha Mei 13.
Pia, mradi huo ukiwa katika mwezi wa tatu wa ujenzi, iliibuka kuwa haukuwa na idhini ya mamlaka ya Mazingira nchini (Nema) lakini wahusika wakuu wakaghushi leseni mnamo Juni 22.
Baada ya tetesi kuzidi, mnamo Julai 21serikali kuu kupitia wizara ya mazingira ilichapisha ombi la ushirikishi umma ili kutoa maoni kuhusu ufaafu wa mradi huo, ikiweka siku 30 kama muda wa harakati hizo.
Chapisho hilo liliwekwa siku ambayo afisa wa utekelezaji mradi huo Bw Ndung’u Njagi alikuwa ameweka kama makataa ya mradi huo kukamilika.