Habari Mseto

Msako mkali Nakuru baada ya wakazi kulishwa paka

June 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na ERCI MATARA

SIKU moja baada ya mwanamume mmoja mjini Nakuru kufungwa jela miaka mitatu kwa kuchinja na kuuza nyama ya paka, maafisa wa afya wameanzisha msako mkali dhidi ya hoteli ambazo hazina leseni.

Jumanne, afisa mkuu wa afya katika Kaunti ya Nakuru, Samuel King’ori alisema hoteli zote pamoja na vichinjio eneo hilo vitachunguzwa upya ili kuhakikisha wenyeji wananunua chakula na nyama salama.

Bw King’ori alisema maafisa wa kaunti hiyo wanawasaka watengezaji sambusa waliokuwa wananunua nyama hiyo ya paka.

Mnamo Jumatatu, James Mukangu Kimani alikiri kortini kuuza nyama ya paka kwa wauzaji sambusa mjini Nakuru.

Kimani alifungwa jela miaka miwili au alipe faini ya Sh200,000 kwa kuchinja paka akiwa na madhumuni ya kuwauzia watu.

Vilevile, Kimani alifungwa jela mwaka mmoja zaidi au faini ya Sh50,000 kwa kuchinja paka maeneo yasiyoruhusiwa.

“Tunachunguza maeneo yote ya kuuzia chakula, na yale ambayo hayana leseni yatafungwa mara moja. Tunawataka wananchi pia watujulishe maeneo ambayo wanashuku yanahusika na vyakula haramu,” alisema Bw King’ori.

Aliwahakikishia wakazi kuwa serikali ya kaunti hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha chakula kinachotumiwa eneo hilo ni salama kwa afya.

Kimani alikamatwa Jumapili baada ya kupatikana akitoa paka ngozi ili kuwasilisha nyama yake kwa mteja wake.

Mfungwa huyo aliwaambia wanahabari kuwa amechinja paka 1,000 na kuuzia watengenezaji sambusa na wenye mikahawa mjini Nakuru tangu 2012.