Msiguse miraa, wakulima wakemea wasomi wa Namlef wanaotaka marufuku
WAKULIMA na wafanyabiashara wa Miraa wamepinga wito wa shirika la Kiislamu wa kuitaka serikali kupiga marufuku biashara hiyo wakisema itawaathiri kimapato.
Walitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Shirika la Kitaifa la Viongozi wa Kiislamu (Namlef) wakisema vita vyao dhidi ya zao hilo vililenga moja kwa moja jamii ya Wameru, ambapo zaidi ya wakazi 700,000 wanaitegemea biashara hiyo.
Walisema miraa ilifanyiwa majaribio na idara mbali mbali za serikali kama vile Nacada na Kemri, kabla ya kutangazwa kuwa ni zao bora na ni makosa kwa Namlef kuwachochea watu dhidi yake.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati ya kupanga bei ya miraa, James Mithika, walisema matamshi ya maafisa wa Namlef ya kutaka kupigwa marufuku kwa biashara ya miraa yalilenga kutenga eneo la Meru.
Alisema kuwa miraa ililetea nchi Sh13.1bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2023/24, na masoko yake makubwa yako katika mataifa yenye Waislamu wengi.
Dkt Mithika ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo chini ya Mamlaka ya Kilimo na Chakula katika Wizara ya Kilimo, alisema serikali inatafuta masoko zaidi ya zao hilo, na Namlef inaweza kulemaza juhudi hizo.
‘Yemen, ambayo ina Waislamu wengi ni watumiaji wa miraa. Djibouti na Wasomali pia ni wateja wetu,” akasema Dkt Mithika.