Habari Mseto

Msiuze chakula, chifu awashauri wakulima

March 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY KIMATU

WAKULIMA katika kijiji cha Nduu katika lokesheni ya Mutituni, Kaunti ya Machakos wameambiwa wasiuze chakula chao baada ya kuvuna mahindi kwa wingi mwezi huu.

Naibu Chifu Mkuu wa lokesheni ndogo ya Nduu, Bw Musyoki Mallei aliwashauri wakulima waanze kupanda vyakula mbalimbali zikiwemo zile za kienyeji zinazoweza kustahimili ukame.

“Ni jambo la maana kuanza kubadilisha upanzi wa vyakula tofauti kila msimu na kujiepusha na kasumba ya kuzoea kupanda mahindi pekee kila msimu. Kumbukeni kuhifadhi chakula mahali mvua na wadudu hawataharibu,” Bw Musyoki akasema.

Bw Musyoki alisema hayo alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika ukumbi wa He was Maendeleo ma Nduu.

Alitoa ushauri kwa wakazi kwamba wawe wakipika chakula kinachowatosha badala ya kutupa chakula kilichobakishwa baada ya watu kushiba.

”Mnaona Kaunti kama ya Turkana, Baringo na kwingineko watu wakila matunda ya msituni yalio na sumu nanyi mnamwaga chakula mlichobakisha mezani. Pikeni kile hakitabaki kitupwe,” akanena.