Msiuze makadamia yenu kwa chini ya Sh100 kwa kilo, serikali yaambia wakulima
SERIKALI imetangaza bei ya chini ya Sh100 kwa kila kilo ya makadamia ili kuzuia wakulima kunyanyaswa na mabroka huku ikitishia kufuta leseni za wanunuzi ambao watakiuka bei hizo.
Hatua hii inafanya zao la makadamia kuwa la hivi punde zaidi kwa serikali kuamua kudhibiti bei hali ambayo imeibua matokeo mseto katika siku za nyuma.
Bidhaa nyingine ambazo imejaribu kudhibiti bei yake ni majani chai, ngano, umeme na mafuta.
Bei ya chini zaidi ya makadamia ilitangazwa na Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Dkt Andrew Karanja mnamo Jumanne.
Hayo yanajiri wakati bei ya zao hilo imeshuka kwa kiasi kikubwa kutokana kupatikana kwa wingi katika soko la kimataifa.
“Bei ya chini ya zao hilo kutoka mashambani ya Sh100 kwa kilo moja itatekelezwa,” Dkt Karanja alisema.
“Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) imepewa jukumu la kutekeleza uzingatiaji madhubuti wa agizo hili, ikiwa ni pamoja na kufuta leseni za wanaokiuka. Mamlaka pia itaongeza ukaguzi na ufuatiliaji ili kuondoa wafanyabiashara wasio waaminifu,” waziri alisema.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya serikali pia kupiga marufuku uvunaji wa makadamia kwa muda wa miezi minne kuanzia Novemba 2, 2024 hadi Machi 1, 2025 ili kuzuia uuzaji wa zao ambalo halijakomaa.
Kwa mujibu wa marufuku hiyo, Wizara pia iliagiza wafanyabiashara wa makadamia kuwasilisha bidhaa zao kwa ukaguzi, uhakiki na kibali ifikapo tarehe Novemba 15, 2024.
Kenya ni mojawapo ya wauzaji wakuu wa makadamia duniani huku zaidi ya asilimia 95 ya makadamia ya humu nchini ikiuzwa katika soko la kimataifa.
Mnamo 2022, Kenya iliorodheshwa kama mzalishaji wa tatu wa makadamia ulimwenguni, nyuma ya Afrika Kusini na Australia.
Wakulima wa Makadamia hata hivyo wamekuwa wakihangaika katika miaka ya hivi majuzi kutokana na bei ya chini inayowalazimu baadhi yao kutelekeza zao hilo na kugeukia mazao yenye faida kuliko makadamia.
IMETAFSIRIWA NA SAMMY KIMATU