Mswada wapendekeza halmashauri mpya kusimamia sekta ya majani chai
Na CHARLES WASONGA
SEKTA ya majani chai nchini itaongozwa na halmashauri mpya ambayo itatekeleza mageuzi yanayolenga kuwezesha wakulima wa zao hilo kupata faida, ikiwa mswada ulioko bungeni utapitishwa na kuwa sheria.
Mswada huo ambao umedhaminiwa na Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot unapendekeza kubuniwa kwa Halmashauri ya Kusimama Sekta ya Majani Chai Nchini (TRAK) itakayobuni kanuni za ustawishaji na mnada wa uuzaji zao hilo ng’ambo.
Asasi hiyo itatwaa mengi ya majukumu yanayoendeshwa na Shirika la Ustawi wa Kilimo cha Majani Chai (KTDA) ambayo wakulima wengi wameilaumu kwa usimamizi uliochangia kupungua kwa faida yao.
Na kwa mara ya kwanza TRAK, ambayo itachukua mahala pa iliyokuwa Bodi ya Chai Nchini (TBK), itazishirikisha serikali za kaunti katika uendeshaji wa usimamizi wa sekta hiyo ambayo iliiletea Kenya Sh140 bilioni mnamo 2018. Bodi hii ni miongoni mwa asasi za kilimo zilizounganishwa kuunda Halmashauri ya Kilimo, Chakula, Samaki (AFFA) mnamo 2014.
Kwa mujibu wa mswada huu, serikali za kaunti ambako majani chai hukuzwa zitasimamia masuala kama; ustawishaji wa majani chai, vita dhidi ya magonjwa ya zao, masoko, vyama vya ushirika na uhifadhi ya udongo na maji.
Bodi ya TRAK inayoongozwa na mwenyekiti ambaye atateuliwa na Rais, kwa ushauri wa Waziri wa Kilimo, na wawakilishi watakaoteuliwa kutoka kaunti saba ambazo hukuza majani chai kwa wingi na Baraza la Magavana (CoG), kulingana na mswada.
Mswada huo ambao ulipitishwa mwaka jana katika bunge la Seneti, teuzi za CoG zitaongozwa na rekodi kuhusu kiwango cha uzalishaji zao hilo katika Shirika la Takwimu Nchini (KBS) kufikia wakati wa uteuzi.
“Wanachama wengine wa bodi ya TRAK watajumuisha mtu moja atakayeteuliwa na chama kinachosheheni wakulima wengi wa majani chai na afisa mkuu mtendaji wa halmashauri hiyo,” kulingana na kipengele cha 10 cha mswada huo.
Mswada huo unaipa mamlaka hiyo nguvu ya usimamizi wa masuala yote katika sekta ya chai; kushirikisha shughuli za watu binafsi na mashirika; na kuwezesha wadau wote katika sekta hiyo kupata manufaa na rasilimali husika katika sekta hii.
Na kwa ushirikiano na Wizara wa Kilimo, TRAK itabuni sera na sheria za kusimamia sekta ya majani chai nchini.
“Mamlaka hii itasajili na kuongoza shughuli za wakulima wa majani chai na viwanda vya utayarishaji zao hili; itatoa leseni kwa wafanyabiashara, wasimamizi wa viwanda vya chai, maajenti na mawakala,” kulingana na kipengele cha 20 cha mswada huo.
Pia itatoa huduma za ushauri kuhusu mbinu za ukuzaji majani chai na uongezaji thamani; itashirikisha utafiti na kuongoza utatuzi wa mizozo ibuka miongoni mwa wadau.
Isitoshe, TRAK itatoa leseni kwa wafanyabiashara na viwanda vya kutayarisha chai pamoja na wakulima. Na sharti wakulima wote wa zao hilo wajisajili na kiwanda fulani, kulingana na mswada huo.
“Na mtu au shirika ambalo litaendesha shughuli za uuzaji majani chai humu nchini kwa njia rejareja au mnada au mataifa ya nje bila leseni kutoka kwa mamlaka ya TRAK atapigwa faini ya Sh1 milioni, kifungo cha miaka miwili gerezani au adhabu zote mbili,” kulingana na kipengee cha 22 cha mswada huo.
Mswada ulijadiliwa wiki jana katika Bunge la Kitaifa na kupata uungwaji mkono kutokana wabunge wa mirengo yote.
Mnamo Alhamisi ujadiliwa tena katika hatua ya tatu, ambapo wabunge watakuwa na fursa ya kujumuisha masuala kadhaa (kupitia marekebisho) kwa lengo la kuuboresha zaidi.