Habari Mseto

Muthama amkashifu Raila kuhusu kura ya maamuzi

May 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

ALIYEKUWA Seneta wa Machakos, Bw Johnstone Muthama amemkashifu vikali kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kwa kusisitiza kuwa kura ya maamuzi itafanyika mwaka huu 2020.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Jumatano asubuhi, Bw Muthama alitaja pendekezo la Bw Odinga kama lisilofaa, hasa wakati huu ambapo nchi inakabiliana na janga la corona.

“Bw Odinga amedhihirisha kwamba anajipenda sana na kujali maslahi yake binafsi. Anapaswa kufahamu kwamba kuna wakati wa kila kitu. Huu ni wakati wa kujadili na kuwasaidia wananchi,” akasema Bw Muthama.

Kauli yake inafuatia matamshi ya Bw Odinga mnamo Jumanne, aliposisitiza kuwa kura ya maamuzi kuigeuza katiba lazima ifanyike mwaka huu.

Wawili hao walikuwa katika muungano wa Nasa, lakini wakakosana, Bw Muthama akimlaumu Bw Odinga kwa kujipenda.

Wakati huo huo, Bw Muthama alidai kwamba chanzo kikuu cha changamoto za kisiasa zinazokikumba Chama cha Jubilee (JP) zinatokana na “mashauri mengi” ambayo Rais Uhuru Kenyatta anapokea kutoka kwa wanasiasa.

Bw Muthama alidai kuwa hatua ya Rais Kenyatta kukubali kushirikiana na wanasiasa kama Bw Odinga na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, ndiyo sababu kuu ya kuyumba kwa jahazi la chama hicho.

“Kabla ya Bw Odinga kubuni ushirikiano na Rais Kenyatta, uhusiano wa Rais na Naibu Rais William Ruto ulikuwa mzuri. Lengo la Raila ni kuhakikisha kuwa amesambaratisha mipango yote ya Jubilee kwa kuwagonganisha wawili hao,” akasema Bw Muthama.