Habari Mseto

Mwanafunzi akamatwa kwa dai alikata binamuye kiganja cha mkono

Na GEORGE ODIWUOR April 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

POLISI Rachuonyo Kusini, Kaunti ya Homa Bay wanamzuilia mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15 anayeshukiwa kumkata binamu yake kiganja cha mkono wa kushoto wakati wa ugomvi Ijumaa asubuhi, Aprili 4, 2025.

Mtuhumiwa, ambaye yuko kidato cha tatu katika shule ya sekondari katika eneo hilo, alikamatwa na wananchi baada ya kutekeleza kitendo hicho kabla ya kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kosele.

Anadaiwa kumshambulia mwanafunzi wa darasa la saba baada ya kutofautiana kuhusu masuala ya kibinafsi.

Kisa hicho kilitokea katika kijiji cha Aolo, eneo la North Kamagak.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa binamu hao walizozana walipokuwa wakijiandaa kutengeneza kifungua kinywa.

Chifu wa eneo la Kawere Magharibi, Bw Daniel Odhiambo, alisema kuwa mtuhumiwa alikuwa na pesa ambazo familia ilikuwa imepanga kununua sukari kwa minajili ya chai ya asubuhi.

Hata hivyo, mtuhumiwa alikataa kutoa pesa hizo kwa familia ili inunue sukari.

“Binamu yao wa kike alimwomba pesa hizo, lakini alimjibu kwa ukali. Mwathiriwa alipojaribu kuingilia kati, alijikuta akishambuliwa,” Bw Odhiambo alisema.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa, ambaye alikasirishwa baada ya kuulizwa pesa, alitumia panga kumshambulia binamu yake.

Bw Odhiambo alisema kuwa kiganja kilichokatwa kilianguka chini.

Mayowe ya mwathiriwa yalivutia majirani ambao walikusanyika nyumbani kuona kilichokuwa kikiendelea.

Wananchi walimshambulia mtuhumiwa kabla ya kumpeleka nyumbani kwa chifu.

“Aliletwa kwangu huku baadhi ya watu wakimpiga. Nililazimika kumsindikiza hadi kituo cha polisi ili kumuokoa kutokana na hasira za wananchi,” alisema Bw Odhiambo.

Alisema kuwa baadaye alitembelea eneo la tukio ili kuthibitisha kilichotokea.

Alibaini kuwa baadhi ya majirani walikuwa tayari wamempeleka mwathiriwa hospitalini kwa huduma za dharura.

Kamanda wa Polisi eneo la Rachuonyo Kusini, Philemon Saera, alisema kuwa kesi hiyo inashughulikiwa na idara ya watoto.

“Tumemzuia mshukiwa, lakini kesi yake itashughulikiwa na maafisa wa ofisi ya watoto,” alisema mkuu huyo wa polisi wa kaunti ndogo.