Habari Mseto

Mwangi Kiunjuri asema madai ya uhai wa Ruto kuwa hatarini ni 'mojawapo ya mbinu katika siasa'

June 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

WAZIRI wa Kilimo Mwangi Kiunjuri Alhamisi ametaja madai kuwa kuna mawaziri ambao wanapanga kumuua DP William Ruto kuwa ya kawaida katika msimu wa siasa.

“Huu ni msimu wa siasa; mengi yapo njiani yakija na utasikia ya kushtua, ya kuchekesha, ya kuudhi na ya kila aina. Nimekuwa kwa siasa kwa muda na ninayaelewa haya maneno,” amesema Kiunjuri.

Ameambia Taifa Leo akizungumza kwa simu: “Mimi sina habari kuhusu njama ya mauaji ya Ruto. Sikuhudhuria mikutano ambayo inadaiwa kuwa iliandaliwa katika La Mada Hotel na sikupata wa kiniarifu yaliyokuwa yakijadiliwa. Kwa kawaida, kile sikushirikishwa siwezi nikawa na urasmi wa kusema washirika walipanga nini.”

Bw Kiunjuri alisema kuwa “ni ukweli kuwa mimi huhusishwa sana na urafiki na Naibu Rais, hili likiwa ni suala la kawaida.”

“Mimi kama waziri ndani ya serikali ya Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto kwa kawaida itanibidi niheshimu hao wawili kama viongozi wangu. Urafiki wangu na Ruto sio wa kisiri, ndio uko,” amesema.

Bw Kiunjuri amesema kuwa ikiwa kuna madai ya kumuua DP Ruto, “basi kuna vile vitengo vya kuwapa Wakenya ukweli na kuzuia ujambazi wa kiwango hicho kutekelezwa sio tu dhidi ya viongozi wa kisiasa, lakini kwa kila Mkenya.”

Kiunjuri amesema kuwa “siasa za urithi wa 2022 zimeingia katika awamu ya ushindani mkuu na ndio sababu kila kuchao kunazuka madai ya kila aina kuhusu karibu kila mtu ndani ya serikali.”

Amesema ushindani huwa ndani ya serikali, ndani ya raia na pia kwa washirika ng’ambo, akisema kuwa yale ambayo hadi sasa yamezuka ni kidogo tu ikilinganishwa na yale mengi na makubwa ambayo yako njiani yakija kupamba ulingo wa siasa.

“Mimi nimeamua kukaa chini ya maji nikiupa uwanja wa kisiasa macho tu na masikio kwa kuwa kufanya hivyo kuna afueni kubwa,” amesema.

Amesema kuwa miaka mitatu ambayo inabakia ili taifa liandae uchaguzi mkuu wa 2022 ni muda mwingi sana na ambao unafaa kutumika kuimarishia Wakenya maisha wala sio kuwaweka katika mijadala ambayo haina uvutio wa maendeleo.

Bw Kiunjuri amesema kuwa “mimi kwa kawaida hupenda maridhiano badala ya malumbano lakini kwa wengine, mbinu ni tofauti…na hizo zote ni siasa.”