• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mwizi aliyekosa sadaka ya kuiba kanisani awarai waumini wamuombee

Mwizi aliyekosa sadaka ya kuiba kanisani awarai waumini wamuombee

NA WAIKWA MAINA

WAKAZI eneo la Engineer, Kaunti ya Nyandarua, wameshangazwa na kisa cha mwizi ambaye aliacha barua yenye ujumbe wa majuto na kuomba msamaha baada ya kuvamia kanisa Jumapili usiku kwa lengo la kuiba sadaka lakini akaambulia patupu.

Mwizi huyo aliyedai alitumwa na mshirika wa kanisa alitoboa shimo kwenye ukuta wa mabati kanisani lakini hakuamini alipoingia ndani kupekua kila mahali na kukosa kupata matoleo ya siku hiyo ya ibada.

Kwenye nakala ya barua aliyoandikia washiriki wa kanisa hilo, mwizi huyo alisikitika kwamba hakuambulia chochote ilhali alidokezewa na muumini huyo kwamba kulikuwa na pesa za uhakika kwenye hazina ya kanisa hilo.

“Wapendwa washiriki wenzangu, kwanza nawasabahi? Nilitumwa hapa na mmoja wenu aliyenipasha kwamba kulikuwa na pesa zilizohifadhiwa ndani ya kanisa. Hata hivyo, sikupata chochote. Mungu awabariki na mniombee, ahsanteni ,” ikasoma barua hiyo kisha akatia saini na kuandika ‘‘barua kutoka kwa mwizi aliyevunja kanisa’’.

Hata hivyo, Kasisi wa kanisa hilo Peter Wanyoike alisema kulikuwa na kiasi fulani cha fedha ndani ya kanisa ambazo zimepotea baada ya tukio hilo.

“Tulipata barua kanisani wakati polisi waliwasili kuanzisha uchunguzi wao. Tunaamini kulikuwa na kiasi fulani cha fedha ndani ya kanisa. Tumemsamehe.”

You can share this post!

Ajuza asimulia korti jinsi mwanawe amekuwa akimcharaza

Mganga aonya pasta kwa kumchomea biashara

adminleo