NAOMI MBURU: Ameng'ang'aniwa na NTV, KTN na Citizen kuigiza
Na JOHN KIMWERE
ANAAMINI anacho kipaji tosha kuzalisha filamu bora na kupata mpenyo kuteuliwa kwenye tuzo za kimataifa za Oscars, Grammys na Emmys.
Ni kati ya wasanii wa kike hapa nchini wanaojivunia kupiga hatua katika sekta ya maigizo. Alianza kushiriki maigizo akisoma shule ya msingi alipokuwa akishiriki michezo ya kuigiza shuleni pia kanisani.
Ni hali iliyomfanikisha kushiriki majaribio siku moja baada ya kumatamisha elimu ya sekondari mwaka 2011.
Tunayezungumzia siyo mwingine bali ni Naomi Mburu ambaye anaelekea kutinga miaka minne akishiriki kipindi cha Tahidi High ambacho hurushwa kupitia Citizen TV.
Binti huyu anayeelekea kutinga umri wa miaka 25 amehitimu kwa shahada ya digrii kuhusu Masuala ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN). Anajivunia kutunukiwa kipaji cha uigizaji na pia utayarishaji wa filamu.
”Hakika nashukuru Mungu ameniwezesha kushiriki filamu nyingi tu ndani ya muda mchache,” alisema na kuongeza kuwa analenga kutinga hadhi ya kimataifa.
Anajivunia kushiriki vipindi kadhaa zilizokuwa zikionyeshwa kupitia vituo tofauti vya runinga hapa nchini ikiwamo ‘Mchungaji – NTV,’ ‘Sumu la Penzi – Maisha Magic,’ ‘Urembo – Maisha Magic,’ na ‘Mother In Law-Citizen TV,’ kati ya zingine.
Aidha anajivunia kuwa kati ya maprodusa waliotengeneza filamu inayokwenda kwa jina ‘GSM –The Parable of Judas’ ambayo huonyeshwa kupitia Kwese TV ya Afrika Kusini baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.
Pia anajivunia kushiriki filamu ya iitwayo My Two Wives ya KTN. Kadhalika chini ya Son of Man International ameshiriki filamu ‘The Lady in Red’ inayotazamiwa kuzinduliwa Jumapili ijayo.
”Nimeanzisha kampuni iitwayo Nay Nay Productions ninapolenga kuzalisha filamu za TV Series kuangazia stori za kweli ambazo baadhi wengi hupitia maishani,” alisema na kuongeza ana imani atafanya vizuri.
Hivi karibuni analenga kuanza kuifanyia kazi filamu ‘Wish Her to Tell’ inayohusu masuala ya kawaida katika jamii. Kisura huyu anasema anapenda kutazama filamu kama ‘The Good Lie’ na ‘The Boy Who Harnessed the Wind’ ambayo huonyeshwa kupitia Netflix.
Kwenye matangazo ya biashara amefanya na Safaricom Twaweza, First Capital Bank na Vuna Tatu – masuala ya kubashiri matokeo ya mechi za soka.
Katika mpango mzima analenga kufanya kazi na mwigizaji wa kimataifa mzawa wa hapa nchini Lupita Nyongo anayetesa kwenye filamu za Hollywood.
”Natoa mwito kwa serikali ipunguze ada ambayo hutoza kampuni za kuzalisha filamu ili kuvutia wawekezaji wa kigeni kufanya shughuli zao hapa nchini kusudi kutoa nafasi za ajira kwa waigizaji wa humu nchini,” alisema.
Anashauri waigizaji chipukizi kutoketi kijiwe kusubiria ajira mbali wajitume kuonyesha ujuzi wao hasa kushuti filamu fupifupi na kuzitupia mitandaoni.
Pia anawahimize wafanye utafiti kuhusu uigizaji ili kunoa talanta zao. Kadhalika anawaomba Wakenya wawape waigizaji wa humu nchini sapoti ndipo wajitahidi kwenye juhudi za kuzalisha filamu bora za hadhi ya kimataifa.