• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
NCIC yanguruma hofu ikitanda kuhusu mkutano wa BBI

NCIC yanguruma hofu ikitanda kuhusu mkutano wa BBI

PETER MBURU Na GEORGE SAYAGIE

TUME Amani na Maridhiano Kitaifa (NCIC) jana ilitoa mwelekeo ambao mikutano ya kupigia debe Mpango wa Maridhiano (BBI) itafuata, ikikosoa mtindo wa viongozi wa kisiasa kutumia mikutano hiyo kutusiana na kujibizana.

Tume hiyo iliwataka waliopewa majukumu ya kuandaa mikutano hiyo kutoacha mchakato huo kuchafuliwa, kwa kuhakikisha kuwa wanaohutubu wanazungumza ukweli na hawaendelezi ajenda ya chuki na utengano.

NCIC ilisema kuwa wanaohutubu wanafaa kufafanulia wananchi ukweli, kueleza palipo na pengo na kupendekeza njia nzuri ya kuboresha, badala ya kuhadaa wananchi.

Vilevile, NCIC iliwatahadharisha wasimamizi wa mikutano ya BBI na viongozi kuwa ndio wataadhibiwa endapo kutaibuka vurugu katika mikutano hiyo, kutoka kwa wafuasi wao.

“Wafuasi pia wataadhibiwa kibinafsi ama kwa jumla kutokana na tabia zao na fujo zozote ambazo wataanzisha,” akasema mwenyekiti wa tume hiyo Samuel Kobia.

Kulingana na NCIC, asasi za kiusalama pia zitahitajika kuhakikisha kuwa kuna usalama wa kutosha wakati wa mikutano hiyo, na kuwalinda Wakenya wote wanaohudhuria.

“Mikutano hiyo inafaa kuwa ya kufurahia ukwasi wetu huku tukiepuka matendo yanayoleta dhana ya kutenganisha,” Dkt Kobia akasema.

Tume hiyo ilitoa habari hiyo wakati baadhi ya wakazi wa Kaunti ya Narok walidai kuingiwa na hofu, kufuatia uvumi kuwa wenyeji ambao si wa kutoka jamii ya Maasai hawataruhusiwa kuhudhuria mkutano wa BBI uliopangwa kaunti hiyo wiki hii.

Uvumi huo ulianza saa chache tu baada ya seneta wa Narok Ledama Ole Kina kusema kuwa mkutano huo wa kesho unalenga kutoa fursa kwa watu wa jamii ya Maasai kuwasilisha mapendekezo yao kwa kamati ya BBI, akisema ni suala linalohusu changamoto za Wamaasai pekee.

Vilevile, ulifuatia kisa cha baadhi ya viongozi wa kaunti zinazomilikiwa na jamii ya Maa ambao si wa jamii hiyo kuzuiwa kuhudhuria kikao cha kupanga mkutano huo wa kesho. Mmoja wa viongozi waliozuiwa ni mbunge wa Kajiado Kaskazini Joseph Manje.

Lakini maafisa wa usalama kaunti hiyo walisema kuwa hali ya usalama itadumishwa na hakuna mkazi atakayezuiwa kuhudhuria.

Katika ujumbe wa NCIC jana, hotuba zote zinazotolewa katika mikutano ya BBI sharti ziepuke matusi ama lugha nyingine ya kudunisha baadhi ya watu ama jamii fulani.

NCIC ilionya kuwa watakaotumia lugha ya aina hiyo wataadhibiwa vikali.

“Kumbukeni kuwa katika haya mazungumzo, mamilioni ya Wakenya wanafuatilia, pamoja na majirani zetu na zaidi ya yote Mungu,” Dkt Kobia akasema.

Kabla ya mikutano kuhusu BBI kukatizwa takriban wiki mbili zilizopita kufuatia kifo cha Rais Mstaafu Daniel Moi, matukio machafu ya viongozi kujibizana, kutusiana na kudhulumiwa mikutanoni yalikuwa yakishuhudiwa, huku wanasiasa wakitumia mikutano hiyo kuendeleza uhasama na tofauti zao za kisiasa badala ya kuelimisha Wakenya.

You can share this post!

Wakenya walio China wasema pesa si muhimu

NHIF yahitaji mageuzi ili kuboresha afya – Kagwe

adminleo