NCPB yapuuza agizo la Uhuru kuhusu mahindi
Na BARNABAS BII
BODI ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) imechelewa kuanza kununua mahindi kutoka kwa wakulima kama alivyoagiza Rais Uhuru Kenyatta ikidai haijapata idhini ya kuagiza magunia yatakayotumiwa kuhifadhi nafaka hiyo.
Rais Kenyatta mapema mwezi huu aliagiza NCPB kuanza kununua mahindi mara moja ili wakulima wapate fedha za kujiendeleza kimaisha na pia kuandaa mashamba kwa msimu mpya.
Hatua hiyo imewadia siku chache baada ya kufichuka kuwa mashirika mengi ya Serikali yamepuuza agizo la Rais Kenyatta mwaka jana kuwa yawe yakichapisha orodha za wanaotuma maombi ya tenda na pia wale wanaopewa tenda hizo.
Bodi ya NCPB imejitetea kuwa inasubiri idhini kutoka kwa Bodi Hifadhi ya Chakula cha Dharura (SFRTF) ndipo inunue magunia hayo. Bodi hiyo inaongozwa na aliyekuwa waziri, Noah Wekesa.
“Bado tunasubiri SFRTF ituruhusu kununua magunia ndipo tuanze kuchukua mahindi kutoka kwa wakulima,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa NCPB, Bw Albin Sang.
Utathmini mpya unaopaswa kufanyiwa wakulima ili kuzuia matapeli katika ununuzi huo pia umekwama kwa sababu hakuna wafanyakazi wa kutosha kufanya kazi hiyo.
Wasimamizi wa NCPB jana walikiri hawajapokea mahindi kutoka kwa wakulima, wiki tatu baada ya Rais Kenyatta kuagiza ununuzi uanze.
Duru katika Wizara ya Kilimo zilisema zabuni za kununua magunia zilikuwa hazijapeanwa kufikia wakati ambapo rais alitoa agizo mahindi yaanze kununuliwa.
“Urasimu uliokita mizizi serikalini ndio unachelewesha utoaji wa fedha kutoka kwa Wizara ya Fedha hadi zifikie NCPB. Idhini itahitajika kutoka kwa maafisa wa Wizara ya Kilimo na SFRTF kabla fedha zifike, na haya yote yanachukua muda mrefu,” akasema afisa wa cheo cha juu katika Wizara ya Kilimo.
Serikali imepanga kununua magunia milioni mbili ya mahindi kwa Sh5 bilioni ambapo kila mkulima atahitajika asipeleke zaidi ya magunia 400 ya mahindi kwa NCPB.