• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 3:16 PM
Ndoa hizi za siri zimeongeza visa vya talaka – CIPK

Ndoa hizi za siri zimeongeza visa vya talaka – CIPK

Mwenyekiti wa CIPK, tawi la Lamu, Ustadh Abubakar Shekuwe akionya wakazi na viongozi wa dini dhidi ya kujihusisha na ufungishaji ndoa za siri eneo hilo. Asema ndoa za siri zinachangia ongezeko la idadi ya talaka zinazotolewa Lamu, hivyo kuzidisha mahangaiko kwa familia. Picha/ Kalume Kazungu

NA KALUME KAZUNGU

BARAZA la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK) tawi la Lamu limeonya viongozi wa kidini na wakazi dhidi ya kujihusisha na ufungaji ndoa za siri eneo hilo bila ya kufuata kanuni za dini.

Mwenyekiti wa CIPK wa Kaunti ya Lamu, Ustadh Abubakar Shekuwe, anasema kuna mtindo uliochipuka katika siku za hivi , ambapo wachumba wamekuwa wakikaidi sheria za dini na badala yake kufunga ndoa kisiri bila ya kuhusisha mashahidi kama inavyohitajika.

Akizungumza na Taifa Leo mjini Lamu, Ustadh Shekuwe alisema ndoa za siri zimechangia migorogo chungu nzima kushuhudiwa miongoni mwa wanadoa punde wanapooana.

Alisema ndoa za siri pia zimechangia ongezeko la talaka zinazopeanwa Lamu.

Ushadh Shekuwe kadhalika aliwaonya wachumba dhidi ya kufungwa ndoa na viongozi wa kidini ambao hawajaidhinishwa kutekeleza huduma hiyo.

“Kuna baadhi ya wachumba ambao wamekuwa wakifuata njia za mkato kufungisha ndoa zao. Wanafanya ndoa kwa usiri mwingi kiasi kwamba hata wazazi wao hawajulishwi. Hayo ni makosa. Ndoa lazima ihusishe walii wa upande wa mwanamke na pia mume.

Walii anaweza kuwa baba au mama mzazi, ndugu, ami au mjomba. Ningewatahadharisha wale wanaofanya ndoa za siri kwamba wanalofanya ni zinaa wala si ndao halali. Pia wajue mtindo huo unaongeza idadi ya talaka zinazopeanwa hapa Lamu,” akasema Ustadh Shekuwe.

Kiongozi huyo wa dini pia aliwataka viongozi wengine halali wa kidini, wakiwemo mashehe na maimamu kususia kufungisha ndoa za siri eneo hilo.

Ustadh Shekuwe aidha aliwataka wanandoa kuheshimiana punde wanapooana kihalali ili kujenga familia dhabiti eneo hilo.

“Wanandoa wanapoachana, watoto huwa ndio wanaoteseka kwa kukosa malezi bora, ikiwemo yale ya baba au mama. Watu waheshimiana katika ndoa zao ili kujenga misingi imara ya familia,” akasema Bw Shekuwe.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa 2017 kutoka kwa ofisi ya CIPK tawi la Lamu, idadi ya talaka iliyoshuhudiwa ilikuwa jumla ya 300 kati ya mwaka 2014 na 2015 na kufikia mwaka jana, visa hivyo vilikuwa vimepungua hadi 10 pekee.

You can share this post!

Baa kuu la njaa lazua utapiamlo na kuumiza wakazi Pokot...

RASMI: Githu amkabidhi Paul Kihara ofisi ya Mwanasheria Mkuu

adminleo