Habari Mseto

Nilitoroka na mahari ya baba ili asioe mchumba wangu, kijana asimulia

October 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na STEPHEN ODUOR

MVULANA wa miaka 17 katika Kaunti ya Tana River, aliyetorosha mahari iliyokusudiwa kutumiwa na babake kuoa mke wa nne, amewaelezea wazee kwamba bi harusi mtarajiwa alikuwa mchumba wake, ndiposa akachukua hatua hiyo.

Mvulana huyo ambaye alirudi nyumbani Jumapili baada ya ushawishi kutoka kwa vijana waliotumwa kumtafuta kichakani alikotorosha ng’ombe waliokuwa watumiwe kulipia mahari, alisema alichukua hatua hiyo baada ya juhudi zake za kushawishi wazee kusimamisha babake asioe mchumba wake kugonga mwamba.

Kulingana na Mzee Hussein Barisa, ambaye aliongoza mchakato wa upatanishi, kijana huyo aliwaeleza kuwa bi harusi tayari ana mimba yake ya miezi mitatu.

“Msichana alikuwa aozwe kwa mzee huyo ili kuiepusha familia yake aibu baada ya wazazi kugundua alikuwa mjamzito nje ya ndoa na hakutaka kumtaja aliyehusika,” alisema Bw Barisa.

“Baada ya kijana kufichua kuhusu uhusiano wake na bi harusi, tulizungumza na babake na tukamwelezea kwamba kweli mwanamke huyo alikuwa na ujauzito wa mtoto wake na alishtuka sana,” alisema.

Kijana naye alisema waliamua kupata ujauzito na mchumbake kama njia ya kumshawishi babake akubali waoane, akidai babake alikuwa na tabia ya kukataa wachumba wake wote.

Sasa mzee huyo wa miaka 74 amekubali mapatano na mwanawe.

Katika mahojiano na Taifa Leo, mzee huyo alisema mtoto wake hakumuarifu kuhusu uhusiano wao na hata kuhusu ujauzito.

Alijitetea kuwa hamu yake ya kumuoa msichana huyo ilikuwa katika juhudi za kuondolea familia yake aibu, jambo alilosema linakubalika kitamaduni.

Baada ya kupatana, mzee huyo amemzawadia mwanawe mahari ya ng’ombe 17 aliotoroka nao awali, na ameahidi kumsaidia yeye na mchumba wake kuoana.

Wawili hao watashiriki katika sherehe ya uchumba kitamaduni mwezi ujao, sherehe itakayoongozwa na wazazi wa pande mbili, kabla ya harusi mwaka ujao.