Nipeni ruhusa nipatanishe Mlima Kenya – Waiguru
Na NDUNGU GACHANE
GAVANA wa Kaunti ya Kirinyaga, Bi Anne Waiguru amejitolea kupatanisha viongozi wa Mlima Kenya ambao wamegawanyika katika mirengo miwili; inayomuunga Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.
Eneo hilo lenye idadi kubwa ya wapigakura ambao wamekuwa wakiungana katika chaguzi za urais, sasa limekumbwa na mkanganyiko kwani kuna viongozi wanaounga mkono azimio la Dkt Ruto kuwania urais 2022, na wengine wanaosisitiza kuwa hataungwa mkono moja kwa moja kutoka kwao.
Gavana huyo ambaye sasa anazungumza lugha sanifu ya Kikuyu akiongezea misemo ya kitamaduni, amesisitiza kuwa atafanya kila awezalo ili kurudisha maelewano kati ya viongozi wa eneo hilo kuunga mkono Rais na handisheki kwa manufaa ya Mlima Kenya.
Bi Waiguru anapanga kufikia kila kiongozi bila kujali upande anaoegemea, iwe ni Kieleweke, Tangatanga au Team Hema inayosimamiwa na Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria ambaye alitangaza atawania urais mwaka wa 2022.
Anatarajia kufanya hivyo kupitia kwa mikutano ya kisiasa na ya wataalamu ili eneo hilo liwe na umoja uliokuwepo awali.
Bi Waiguru yuko kwenye orodha ya viongozi wanaoaminika kuwa na nia ya kumrithi Rais Kenyatta na kuongoza Mlima Kenya kisiasa kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Wengine ni Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri, na aliyekuwa Mbunge wa Gatanga, Bw Peter Kenneth ambaye pia aliwania urais mwaka wa 2013.
Alipozungumza mjini Kenol, Ijumaa iliyopita wakati wa mkutano wa hadhara wa kikundi cha viongozi wa kike wa kisiasa cha Embrace, gavana huyo alisema inahitajika viongozi wa eneo hilo waungane na wawe na msimamo mmoja kwa manufaa ya maendeleo na malengo ya kisiasa.
“Sitakaa kitako na kutazama viongozi wakibomoa nyumba yetu. Huenda tuna matatizo lakini hatufai kuharibu kile ambacho kimetuunganisha kwa miongo mingi kwa ajili ya mgeni ambaye anahitaji tu kura zetu. Hakuna mtu anayeelewa mahitaji ya eneo hili kama Rais Uhuru Kenyatta na inafaa tumuunge mkono na kumpa mazingira bora ya kufanyia wananchi kazi,” akasema gavana huyo.
Alisisitiza kuwa Rais bado ndiye kigogo wa kisiasa katika eneo hilo na atakuwa na usemi mkubwa kuhusu yule anayestahili kuungwa mkono kwa urais Mlima Kenya.
Alikumbusha viongozi kwamba ni mwenyeji pekee anayeweza kuwapatanisha wala si mgeni asiyefahamu masuala yao ya ndani.