• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Nisaidieni kukabili wanaomezea mate kiti changu, gavana awalilia madiwani

Nisaidieni kukabili wanaomezea mate kiti changu, gavana awalilia madiwani

NA DERICK LUVEGA

GAVANA wa Vihiga Dkt Wilber Ottichilo amewaagiza madiwani katika kaunti yake kutumia mikutano ya umma kumtetea dhidi ya wapinzani wake wanaomezea mate ugavana wa kaunti hiyo.

Dkt Ottichilo ameamua kukumbatia mbinu hiyo baada ya kulemewa na shutuma za wapinzani wake anaodai wamekuwa wakidanganya raia kwamba serikali yake imezembea katika utoaji wa huduma.

Haya yanajiri baada ya mtangulizi wake Moses Akaranga kutangaza kwamba atakuwa debeni 2022 akilenga kutwaa kiti hicho kwa mara nyingine ili kufanikisha ajenda yake ya maendeleo kwa raia wa Vihiga.

Vilevile duru zinaarifu kwamba Seneta George Khaniri na Mbunge wa Sabatia Alfred Agoi wanamezea mate wadhifa huo ingawa wawili hao bado hawajatangaza uwaniaji wao hadharani.

Mabw Khaniri na Agoi wamekuwa mstari wa mbele kukosoa uongozi wa Dkt Ottichillo na uwaniaji hao utakuwa mwiba kwa umaarufu wa gavana huyo ikingatiwa walimpigia debe kwenye uchaguzi wa 2017.

Ingawa alijinadi kama aliyeleta mabadiliko mengi tangu achukue usukani, Gavana huyo aliwaomba wasimamizi hao kutangaza sifa zake kuhusu mabadiliko mashinani ili raia wasihadaike na kuamini madai ya wapinzani wake.

“Wasimamizi wa wadi ndio wawakilishi wa gavana nyanjani. Lazima mchukue majukumu yenu kwa uzito unaostahili na kueleza raia hatua zilizopigwa na serikali yangu tangu nichaguliwe,” akasema Dkt Ottichilo.

Aidha alisema amewaagiza mawaziri wa kaunti na maafisa wakuu wa kaunti kuangalia maslahi ya wasimamizi hao wa wadi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Kama serikali ya kaunti tunafanya mambo kulingana na sheria. Huwa inachukua muda kuweka mambo sawa na ni kweli kuna watu huko nje ambao hawana subira,” akaongeza Dkt Ottichilo.

You can share this post!

Thamini wateja wako, mkuu wa Username ashauri baada ya tuzo

Kocha wa Mutomo akisifia kikosi chake

adminleo