Njaa yatishia kusababisha vita Kaskazini mwa Kenya
Na JACOB WALTER
WAKAZI wa maeneo ya Kaskazini mwa Kenya wanakabiliwa na tishio la baa la njaa ambayo huenda ikasabisha mapigano ya kikabila, serikali imeonya.
Naibu Kamishna wa Horr Kaskazini Silvester Mwangulu jana alisema kuwa ukame unaoendelea kushuhudiwa katika eneo hilo umeanza kusababisha uhaba wa chakula.
“Tunaomba mamlaka husika pamoja na wahisani kuanza kuweka mikakati ya kusaidia waathiriwa wa baa la njaa ili kuepusha mapigano ambayo huenda yakashuhudiwa,” akasema Bw Mwangulu.
Akizungumza katika Kituo cha Polisi cha Darate wakati wa mkutano wa amani katika Wadi ya Dukana, Bw Mwangalu alisema kuwa ukame umeathiri shughuli za kiuchumi na kilimo katika maeneo hayo.
Alisema malisho yameisha katika maeneo ya Moite, Gas, Sabarei na Sibiloi na wafugaji wameanza kuhamia maeneo ya kusini mwa Ethiopia kulisha mifugo wao.
Kamishna huyo alisema kuwa wafugaji hao huenda wakasababisha mapigano katika maeneo wanakohamia.
Kamishna pia alielezea wasiwasi wake kuwa huenda idadi kubwa ya watoto wakakosa kurejea shuleni mwezi Januari mwaka ujao kwani wataenda na wazazi wao nchini Ethiopia.