Njama ya kuuza kampuni za majani chai kisiri yaanikwa
BARNABAS BII na TOM MATOKE
VIONGOZI katika maeneo yanayotegemea kilimo cha majani chai Rift Valley, wamedai kuna njama ya watu fulani wenye ushawishi nchini kununua mashamba na kampuni za kimataifa za majani chai ambazo muda wake wa kuendeleza biashara nchini umekamilika.
Viongozi hao kutoka Kaunti za Nandi na Kericho wamedai kwamba watu hao wamekuwa wakifanya mikutano kisiri na wasimamizi wa kampuni husika kujadiliana kuhusu jinsi watanunua kampuni hizo kwa bei ya chini.
Wakiongozwa na Mbunge wa Nandi Hills, Bw Alfred Keter, viongozi hao Jumapili waliapa kuhakikisha kampuni hizoo zitauziwa jamii na kusimamiwa na serikali za kaunti.
“Hatutaruhusu watu wachache kununua mashamba makubwa kwa bei ya chini na kuacha jamii taabani ilhali jamii hizi zilifurushwa kutoka kwa ardhi zao kutoa nafasi kwa mashamba hayo,” akasema Bw Keter.
Gavana Paul Chepkwony alitoa wito kuanzishwe kampuni ya umma itakayosimamia viwanda vya majanichai ambavyo kandarasi zao za miaka 99 imekamilika ili usimamizi uwe mikononi mwa umma.
“Makampuni ambayo kandarasi zao za kukodisha ardhi zimekamilika na kufutiliwa mbali yanafaa kuachia kaunti usimamizi kwa manufaa ya watu wetu,” akasema Prof Chepkwony.
Ameanzisha mikakati ya kushtaki Serikali ya Uingereza kwa ukatili uliotendwa dhidi ya jamii ya Wakipsigis ikiwemo kuhamishwa kwa lazima ili watoe nafasi kwa mashamba makubwa ya majanichai.
Chama cha Wafanyakazi wa Mashamba Makubwa Kenya (KPAWU) kimeunga mkono wito wa viongozi wa maeneo hayo kutwaa usimamizi wa makampuni hayo ya majanichai ili kuzuia uwezekano wa janga la ukosefu wa ajira.
Makampuni mengi aina hiyo yako katika Kaunti za Nandi, Kericho, Bomet, Murang’a na Kiambu humu nchini.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Wapandaji Majanichai Kenya, Bw Apollo Kiarie, alisema makampuni mengi ya kutengeneza majanichai yameshindwa kutumia uwekezaji wa mamilioni ya pesa kwa sababu ya mizozo kuhusu kandarasi zao wanazotaka zitolewe upya.
“Si haki kwa serikali za kaunti kukataa kutoa upya kandarasi za kukodisha mashamba zilizopitwa na wakati ikizingatiwa kuwa sekta hii huletea nchi mapato mengi ya kigeni,” akasema Bw Kiarie.
Kwa miaka michache sasa, sekta ya majanichai imekuwa ikipata hasara kwa sababu ya hali mbaya ya hewa na bei ya chini ya zao hilo katika soko la kimataifa.