NYS: Agizo DPP atenganishe kesi kumi mara tatu
Na Richard Munguti
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji Jumanne aliamriwa atenganishe mara tatu kesi kumi za kashfa ya Sh469milioni zilizoibwa kutoka kwa Shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu Bi Lilian Omollo na washukiwa wengine 50.
Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi (ACC) Bw Douglas Ogoti alimwamuru DPP awasilishe ushahidi pasi na kuchelewa katika kesi hii iliyo na umuhimu wa kitaifa.
Bw Ogoti aliagiza DPP aanze kuwasilisha ushahidi Oktoba 29 2018 na kuendelea pasi kusitishwa hadi Desemba 7 2018. Hakimu alimwamuru DPP atenganishe kesi hizo ziwe tatu na kumtaka awasilishe mashtaka mapya dhidi ya washukiwa katika kesi hizo.
“ Kesi hii imeahirishwa mara tatu ili DPP awe na muda wa kuwapa washukiwa ushahidi lakini hili limeshindikana.Lazima nichukue msimamo kama korti na kutoa mwelekeo. Lazima kesi ianze kusikizwa Oktoba 29, 2018,” akasema Bw Ogoti.
Pia alimtaka DPP aendelee na kupokea ushahidi mpya na mapendekezo ya washukiwa wanaotaka kesi zao zilisuluhishwe nje ya mahakama.
Hakimu alisema ikiwa kuna makubaliano yoyote kati ya DPP na washtakiwa yanapasa kuwasilishwa kortini kwa njia ya maandishi.
“Sitapinga washtakiwa kufika kwa DPP kuungama waliyotenda kuhusu kashfa hii, lakini hili halitamzuia DPP kuwasilisha ushahidi.” Bw Ogoti.
Alimtaka DPP awashtaki washukiwa ambao hawajafika kortini. Hakimu alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamishi makali kutoka kwa mawakili wanaowatetea Bi Omollo, aliyekuwa mkurugenzi wa NYS Bw Richard Ndubai pamoja na washukiwa wengine kuwa “DPP hana pupa tena ya kuendelea na kesi hiyo kinyume cha kasi washtakiwa walivyokamatwa na kufikishwa kortini.”
Mawakili Cliff Ombeta, Kirathe Wandugi na Assa Nyakundi waliongoza mawakili 39 kulalamika kuwa DPP “anakandamiza haki za washtakiwa waliofikishwa kortini pasi kupewa nafasi ya kupumua walipotiwa nguvuni.”
“Washtakiwa walikuwa wanatiwa nguvuni kwa sarakasi ambayo wao wenyewe hawakufahamu kwani walikuwa wanaona kama ni filamu wanatazama filamu,” alisema Bw Wandugi. Wakili huyo alisema vyomba vya habari vya humu nchini na kitaifa zilifurika mahakamani na kupeperusha kushikwa na kushtakiwa kwa washukiwa hao 50.
Bw Ombeta alimweleza hakimu kuwa jambo la kushangaza ni kuwa afisi ya DPP haijawapa nakala za mashahidi licha ya wao kupeleka makaratasi rimu 10 kutengeneza nakala za mashahidi.
Bw Ombeta alisema kuwa kuna kesi kumi dhidi ya washukiwa miongoni mwao familia ya watu watano wa Mzee Ngirita waliofikishwa kortini wote mama na bintize watatu na mwanao.
“Bado hatujapewa nakala za mashahidi. Kuna mashtaka 147 na faili za kesi hii ni 10. Kila faili inatakiwa kutenganisha ndipo kila kesi iendelee kivyake,” alisema Bw Ombeta.
Alilalamika kuwa kesi hiyo imetajwa mara tatu lakini viongozi wa mashtaka Bi Emily Kamau na Bw Alexander Muteti wameshindwa kuwapa nakala za mashahidi na “ hata kuna washukiwa watano bado kushikwa na kushtakiwa kortini.”
Bi Kamau aliomba muda wa siku 21 kukamilisha uchunguzi na kuwakabidhi washtakiwa ushahidi akiongeza , “baadhi ya washtakiwa wanaomba muda wasikizane na DPP ndipo kesi dhidi yao ziondolewe.”