Habari MsetoSiasa

OBADO ABANWA: Ahojiwa kwa saa saba na kuchukuliwa sambuli za DNA

September 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

GAVANA wa Kaunti ya Migori, Okoth Obado, Jumanne alijipata kwenye kona alipohojiwa mchana kutwa na wapelelezi wanaochunguza mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno.

Gavana huyo pia alipeana chembechembe za mwili wake ili ziende kufanyiwa uchunguzi wa DNA huku wapelelezi wakifikia kilele cha uchunguzi wa mauaji ya kikatili wiki iliyopita ya mwanamke huyo.

Msaidizi wake wa kibinafsi Michael Oyamo naye aliachiliwa kwa sekunde chache kabla ya kukamatwa tena.

Mahakama ilikuwa imeagiza Oyamo aachiliwe iwapo hangekuwa amefikishwa kortini saa tatu asubuhi jana. Ndiposa polisi wakamwachilia kwa muda mfupi lakini alipofika tu nje ya kituo cha polisi akanaswa na maafisa waliokuwa wanamsubiri nje wakiwa wamevaa kiraia.

Bw Obado alifika katika makao makuu ya idara ya upelelezi eneo la Nyanza mjini Kisumu mwendo wa saa nne asubuhi na kuelekea moja kwa moja kuhojiwa.

Aliwasili akiwa katika msafara wa magari matatu huku walinzi wake wakizuiwa kuingia na kuagizwa kumngoja nje ya makao ya polisi.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai George Kinoti alisema Bw Obado alifanyiwa uchunguzi wa DNA kuthibitisha iwapo alihusika na mauaji ya Sharon, ambaye alikuwa mja mzito.

Gavana Obado alitajwa tangu mwanzo kuhusiana na mauaji hayo ambapo Sharon alitekwa pamoja na mwanahabari Barrack Oduori wa Nation Media Group kabla ya mwili wake kupatikana umetupwa msituni Homa Bay. Oduor alifanikiwa kuponyoka kwa kuruka kwenye gari la watekaji.

Kutajwa kwake kulitokana na madai alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke huyo.

Uchunguzi wa maiti ya Sharon ulionyesha alipitia mateso makubwa kabla ya kuaga dunia ikiwemo kubakwa na watu kadhaa pamoja na kudungwa kisu mara nane.

Jana, Bw Oduor alifikishwa katika ofisi za idara ya upelelezi kuhojiwa zaidi kuhusu kisa hicho.

Bw Oyamo anatarajiwa kushtakiwa upya katika mahakama ya Nairobi, kwa mujibu wa maafisa wanaoendesha kesi hiyo.

Mwendo wa saa kumi na mbili na dakika kumi jioni, maafisa wa upelelezi waliondoka katika ofisi za upelelezi mjini Kisumu.

Mawakili wake Cliff Ombetta na Roger Sagana walisema Gavana huyo alishirikiana na wapelelezi na kwamba atajitetea dhidi ya madai yoyote yatakayomkabili.

Nguo ambazo Bw Oduor alikuwa amevalia aliporuka kutoka gari la watekaji nyara pia zilichukuliwa na wapelelezi ili kusaidia katika uchunguzi.

Mwili wa Sharon ulipatikana eneo la Obisa karibu na daraja la Owade.

Kifo chake kilikasirisha watu kote nchini huku wanaharakati, wanafunzi wenzake na wanasiasa wakitaka haki itendeke.

RIPOTI ZA BENSON MATHEKA, VICTOR RABALLA NA RUSHDIE OUDIA