Obama kukutana na Uhuru na Raila
Na CECIL ODONGO
ALIYEKUWA rais wa Amerika Barack Obama atafanya kikao na rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwenye ziara yake nchini mnamo Jumatatu.
Kwa mujibu wa dadake Dkt Auma Obama, kiongozi huyo ambaye babake alikuwa Mkenya na mamake raia wa Amerika amekuwa akifuatilia kwa karibu masuala mbalimbali nchini.
Aliongeza kuwa ziara yake imetimia wakati mwafaka baada ya viongozi hao waliotofautiana vikali kuridhiana kufuatia kipindi cha uchaguzi uliojaa uhasama.
Hata hivyo, Bi Obama alikataa kuzungumzia matayarisho ya ziara hiyo ya siku mbili na maswala yatakayojadiliwa kwenye mikutano inayotarajiwa akitaja sababu za kiusalama na kuahidi wanahabari kwamba taarifa kamili itatolewa na afisi ya Rais kupitia msemaji mkuu wa serikali.
“Siwezi kujua kile atakachozungumza atakapokutana na viongozi wakuu nchini wala sijui ataandamana na kiongozi yupi maarufu ila nafahamu kwamba amekuwa akifuatilia kwa makini matukio nchini na ziara hii kwa bahati nzuri inakuja wakati kuna maridhiano nchini,” akasema Bi Obama huku akikosa kuthibitisha iwapo nduguye ataandamana na muigizaji maarufu duniani Oprah Winfrey
Bi Obama alisema nduguye atafungua rasmi kituo alichoanzisha cha Sauti Kuu ambacho ujenzi wake umekuwa ukiendelea tangu 2009 na kimekuwa kikiwapa usaidizi watoto na familia katika kijiji cha Kogelo na kaunti nzima ya Siaya.
Kituo hicho kikubwa kilichojengwa kupitia ufadhili wa mashirika ya kigeni kimekuwa kikiendesha mafunzo kwa wakazi jinsi ya kujikimu kimaisha na kukuza talanta kwenye fani ya michezo kwa kushirikiana na ligi maarufu kama ligi kuu nchini Uingereaza.
“Sauti Kuu ni kituo kinachowapa mafunzo wanajamii kuhusu jinsi watakavyotumia rasilimali zao kutokomeza umaskini, kuyafadhili masomo ya wanafunzi vyuoni na kuwapa ujuzi wa kiufundi wanajamii ili waimarishe mapato yao,” akasema Bi Auma.
Aidha, kituo hicho kinajihusisha na miradi kama utunzaji wa misitu katika Kaunti ya Siaya, kuendesha vita vikali dhidi ya maambukizi ya Ukimwi na kupigana na utamaduni na mila potovu katika jamii.
Rais Obama anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu na atapitia mji wa Kisumu kabla kuelekea Kaunti ya Siaya kufungua kituo hicho. Ratiba kamili ya ziara yake inatarajiwa kutolewa na serikali.
Bw Obama alitembelea Kenya katika kipindi cha pili cha uongozi wake mnamo 2015 lakini hakuweza kufika Kogelo kutokana na kile kilidaiwa kuwa sababu za kiusalama.
Hata hivyo alitoa ahadi wakati huo kwamba angeitembelea Kenya na Afrika Mashariki baada ya kung’atuka mamlakani na kuwa raia wa kawaida.