ODM wasema sasa wako tayari kufanya uchaguzi mashinani
CHAMA cha ODM kimetangaza kuwa kitaendelea na uchaguzi wake wa mashinani kuanzia Novemba 27.
Uchaguzi huo ulistahili kufanyika mnamo Aprili mwaka huu lakini ukaahirishwa kutokana na mafuriko maeneo mbalimbali nchini.
Mwenyekiti wa Kamati Shirikishi ya Kitaifa ya Uchaguzi wa ODM Emily Awita, alisema kuwa chama hicho kiko tayari kuendelea na uchaguzi huo, akisema kura zitapigwa katika kaunti zote 47.
“Jinsi wanachama wote wanavyofahamu NECC kwa mujibu wa katiba, chama iliahirisha kura za mashinani ambazo zilikuwa ziandaliwe mnamo Aprili kutokana na mafuriko maeneo mbalimbali nchini,
“NEC sasa imeafikiana uchaguzi huo wa mashinani uandaliwe Novemba 27 katika vituo vyote vya upigaji kura katika kaunti zote 47,” akasema.
Bi Awita alisema wanachama watawachagua viongozi kupitia makubaliano, kura za moja kwa moja au kuinua mikono na kuwathibitisha wawaniaji wanaowaunga mkono kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane mchana siku ya kupiga kura.
NECC ilitangaza kuwa kutakuwa na uchaguzi wa maafisa 30 wa chama, ambapo 10 watatoka kwenye kila kamati katika kituo cha kupigia kura ambacho kina kamati tatu.
Nyadhifa ambazo zitawaniwa uenyekiti, naibu mwenyekiti, katibu, katibu mtendaji, mwekahazina, kiongozi wa wanawake, kiongozi wa vijana na wanachama watatu.