Habari MsetoSiasa

Oparanya abwaga wanne kuongoza kundi la magavana

January 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

GAVANA wa Kakamega Wycliffe Oparanya Jumatatu alichaguliwa mwenyekiti mpya wa Baraza la Magavana (CoG) kwenye uchaguzi uliofanyika jijini Nairobi.

Gavana huyo aliibuka mshindi kwa kuwashinda wenzake Anne Waiguru (Kirinyaga), Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Salim Mvurya (Kwale) na Jackson Mandago (Uasin Gishu).

Bw Oparanya, ambaye pia Naibu Kiongozi wa chama cha ODM, alichukua mahali pa Gavana Josephat Nanok wa Turkana, aliyekuwa amehudumu kwa muhula mmoja wa miaka miwili.

Kufuatia uchaguzi huo, Gavana Mwangi wa Iria wa Kaunti ya Murang’a alichaguliwa Naibu Mwenyekiti. Alichukua mahali pa Bi Waiguru.

Aliyekuwa gavana wa Bomet, Isaac Ruto, ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kwanza, ambapo alihudumu kati ya 2013 na 2015. Alifuatwa na Waziri wa Biashara na Viwanda Peter Munya, wakati huo akihudumu kama gavana wa Kaunti ya Meru.

Akihutubu mara tu baada ya kuchaguliwa kwake, Bw Oparanya aliwashukuru magavana wenzake, akiahidi kuwa lengo lake kuu litakuwa kushinikiza kuongezwa kwa mgao wa fedha za serikali za kaunti kutoka serikali ya kitaifa.

Bw Oparanya alisema kwamba ingawa Serikali Kuu imekuwa ikijitahidi kuongeza mgao huo, kaunti zingali zinahitaji fedha nyingi ili kufadhili miradi mingi ya maendeleo.

“Asilimia kubwa ya fedha tunazopata kutoka kwa Hazina ya Kitaifa huwa zinatumika kulipia mishahara ya wafanyakazi. Tunaiomba Serikali ya Kitaifa kutuongeza fedha zaidi ili kuhakikisha kuwa tunapata pesa za kutosha kufadhili miradi hiyo,” akasema.

Kwenye taarifa, chama cha ODM kilisifu kuchaguliwa kwake kikisema kwamba hilo linatokana na utendakazi wake mwema.

“Tunampongeza Bw Oparanya kwa kuchaguliwa kwake. Kwa miaka sita aliyohudumu kama gavana, ameonyesha utendakazi mwema kwa kuanzisha miradi muhimu ambayo imechangia sana katika ustawi wa maendeleo wa Kaunti ya Kakamega,” akasema Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna.

Kwa upande wake, Bw Iria aliwaomba magavana kuanza vita vikali dhidi ya ufisadi katika kaunti, kwani umekuwa ukikwamisha baadhi ya mipango muhimu.